KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, March 10, 2011

Mosha abwaga manyanga Yanga



HALI ndani ya klabu ya Yanga imeendelea kuchafuka baada ya Makamu Mwenyekiti, Davis Mosha kuandika barua ya kujiuzulu wadhifa huo.
Taarifa za kuaminika zilizopatikana jana na kuthibitishwa na kiongozi mmoja wa juu wa Yanga zimeeleza kuwa, Mosha aliwasilisha barua hiyo juzi.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Mosha amefikia uamuzi huo kutokana na kuzuka tena kwa hali ya kutokuelewana kati yake na Mwenyekiti, Llyod Nchunga na mfadhili mkuu wa klabu hiyo, Yusuf Manji.
Mosha ametangaza uamuzi wake huo siku chache baada ya kurejea nchini kutoka Uingereza na kushirikiana na viongozi wenzake wa Yanga katika kuiandaa timu kwa ajili ya mechi yao dhidi ya Simba.
Makamu Mwenyekiti huyo, ambaye imeelezwa kuwa ana nguvu kubwa ya kulinyima raha kundi la Friends of Simba, amekuwa haelewani na Nchunga licha ya kukutanishwa mara kadhaa kwa lengo la kumaliza tofauti zao.
Habari zaidi zimeeleza kuwa, Mosha aliandika barua hiyo baada ya kupata shinikizo kubwa kutoka kwa wajumbe wa kamati, kufuatia uamuzi wao wa kubariki kujitoa kwa Manji kuifadhili klabu hiyo.
Imeelezwa kuwa katika kikao cha kumjadili Manji, Mosha alionekana kuwa na msimamo mkali wa kutaka uongozi usimpigie magoti mfadhili huyo, ambao ulipingwa vikali na Nchunga.
Yanga imejikuta ikiingia kwenye mzozo mwingine mkubwa baada ya Manji kuandika barua ya kujiuzulu kwa kile alichodai, kuandamwa na kashfa za kuihujumu timu hiyo.
Uamuzi huo wa Manji umeugawa uongozi wa klabu hiyo katika makundi mawili, ambapo moja linaupinga na kumtaka arejee wakati lingine limebariki kuondoka kwake na kutaka asinyenyekewe.
“Mosha ameamua kuachia ngazi ili kulinda heshima yake na kumwacha Nchunga afanye anavyotaka,” kimesema chanzo cha habari.
Kuna habari kuwa, huenda wajumbe wengine zaidi wa kamati ya utendaji ya Yanga wakatangaza kujiuzulu, kufuatia kubainika kuwepo kwa mipango ya kuwatimua kwenye uongozi watu wanaompinga Manji.
Juhudi za kumtafuta Nchunga ili athibitishe taarifa hizo, hazikufanikiwa jana kwa vile kila alipopigiwa simu yake ya mkononi, haikuwa na majibu.

No comments:

Post a Comment