'
Wednesday, March 30, 2011
SIMBA: Lazima tuivue ubingwa TP Mazembe
WACHEZAJI wa timu ya soka ya Simba wamejigamba kuwa, lazima waifunge TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na kusonga mbele katika michuano ya klabu bingwa Afrika. Wakizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam juzi, wachezaji hao walisema wamepania kuishinda TP Mazembe na kuweka rekodi ya kuivua ubingwa wa Afrika. Majigambo hayo ya Simba yamekuja siku chache baada ya timu hiyo kubanwa mbavu na Kagera Sugar kwa kulazimishwa kutoka nayo suluhu katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Simba na TP Mazembe zinatarajiwa kurudiana Jumapili katika mechi ya raundi ya pili, itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Katika mechi ya awali, iliyochezwa wiki iliyopita mjini Lubumbashi, TP Mazembe iliichapa Simba mabao 3-1. Ili isonge mbele, Simba italazimika kushinda mechi hiyo kwa mabao 2-0. Akizungumzia mechi hiyo, kiungo Mohamed Banka alisema wamedhamiria kupambana kufa au kupona ili kushinda mechi hiyo na kusonga mbele. Banka alisema iwapo Simba iliweze kuivua ubingwa Zamalek mwanzoni mwa miaka ya 1990, haoni kwa nini washindwe kufanya hivyo kwa TP Mazembe. “Ni kweli tumeshindwa kucheza vizuri dhidi ya Kagera Sugar leo (juzi), lakini ni kwa sababu ya mazoezi magumu tuliyopata kutoka kwa makocha wetu. Tuna hakika Jumapili tutakuwa fiti kabisa,”alisema. Beki Amir Maftah alisema, wameshazifahamu vyema mbinu zote za wapinzani wao, hivyo ushindi katika mechi hiyo ni kitu cha lazima. Maftah alisema wana imani kubwa ya kushinda mechi hiyo kwa vile watakuwa wakicheza kwenye uwanja wao wa nyumbani na mbele ya mashabiki wao. “TP Mazembe waje tu, lakini wajue wazi kwamba lazima wafe,”alijigamba beki huyo wa zamani wa Yanga. Kiungo Patrick Ochan kutoka Uganda aliisifu TP Mazembe kwamba ni timu nzuri, lakini alijigamba kuwa, haina nafasi ya kushinda tena mechi ya marudiano. Alisema moja ya mapungufu waliyoyabaini katika kikosi cha TP Mazembe ni ubutu wa safu yake ya ulinzi, hivyo wamejiandaa vyema kuutumia ili kupata ushindi. Ochan alisema watajihidi kuingia eneo la wapinzani wao mara kwa mara ili kuwachosha mabeki wao na hatimaye kufunga mabao ya kushtukiza. Kipa Juma Kaseja alisema, licha ya kufungwa katika mechi ya awali, bado hawajakata tamaa kwa vile nafasi ya ushindi kwao ni kubwa. Amewataka mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi kushuhudia mechi hiyo kwa vile watapata burudani, ambayo hawataisahau kwa muda mrefu. Alisema uzuri wa TP Mazembe hauwezi kuwakwaza kwa vile katika soka lolote linaweza kutokea, lakini cha msingi ni wachezaji kucheza kwa ari na kujituma. Mshambuliaji Emmanuel Okwi alisema wamepania kuifunga TP Mazembe kwa sababu ni timu ya kawaida na wana uwezo wa kuimudu. Hata hivyo, Okwi alisema ili waweze kufanikisha azma yao hiyo, wanapaswa kucheza kwa kujituma na kutambua majukumu yao uwanjani. “TP Mazembe ni timu ya kawaida tu, tuliwakimbiza sana kipindi cha pili kule kwao, kama tukifanya hivyo Jumapili, sioni kwa nini tushindwe kuwafunga,”alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment