KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, March 24, 2011

MOLA WALAZE PEPONI WASANII WA FIVE STARS MODERN TAARAB


KWA kawaida, hakuna binadamu anayependa kifo. Ni kwa sababu kinaogopesha. Kila binadamu anapenda aishi kwa muda mrefu ili ayafurahie maisha hata kama anaishi kwa dhiki na mashaka.
Lakini hakuna mwenye uwezo wa kukipwepa kifo kwani hata vitabu vyote viwili vya Quraan na Biblia vinatamka wazi kwamba, sisi sote ni waja wa Mwenyezi Mungu na kwake ni lazima tutarejea. Kwamba kila chenye roho lazima kionje mauti.
Ishi utakavyoishi, uwe tajiri, masikini, mwanamichezo, mwanamuziki, jambazi atoaye roho za watu ama vyovyote vile, lazima ukumbane na kifo kwa sababu hakikwepeki.
Enzi za uhai wake, rafiki yangu marehemu Remmy Ongala aliwahi kutunga nyimbo nyingi zinazozungumzia kifo, akikilalamikia kwa kuwatenganisha waliopendana, kuwatoa duniani vipofu na walemavu na mengineyo mengi.
Alitamani kila mtu angekuwa akipewa taarifa ya siku yake ya kufa ili aandae sherehe na kuwaaga ndugu na jamaa zake na ikiwezekana kujipeleka mwenyewe kaburini, lakini hilo haliwezekani. Ni siri kubwa iliyofichwa na Mola wetu.
Hivyo ndivyo ilivyotokea kwa wasanii 13 wa kikundi cha taarab cha Five Stars cha mjini Dar es Salaam, waliofariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea usiku wa kuamzia juzi maeneo ya Mikumi mkoani Morogoro.
Katika ajali hiyo, iliyowahuzunisha watanzania wengi, hasa mashabiki wa muziki wa taarab, watu saba walijeruhiwa, mmoja kati yao hali yake ikiwa mbaya.
Ajali hiyo ilitokea saa mbili usiku wakati wasanii wa kikundi hicho walipokuwa wakirejea mjini Dar es Salaam kwa basi aina ya Toyota Coaster, wakitokea katika ziara ya maonyesho kadhaa katika miji ya Ruvuma, Morogoro na Mbeya. Basi hilo lilipata ajali baada ya kuacha njia na kugonga lori la mbao lililokuwa limeegeshwa kando ya barabara baada ya dereva wake kukwepa kukutana uso kwa uso na lori lingine lililokuwa likija upande wake.
Miongoni mwa wasanii waliopoteza maisha yao kutokana na ajali hiyo ni pamoja na mwimbaji nyota wa kundi hilo, Issa Kijoti na kiongozi wake, Nassoro Madenge.
Wengine ni waimbaji Husna Mapande na Hamisa Omary, ambaye ni mke wa msanii Mussa Mipango, mpiga solo Sheba Juma, mpiga gita la besi Omary Hashim, mbeba vyombo Omary maarufu kama Tall, mfanyakazi wa kundi hilo, Ngereza Hassan, wapiga kinanda Tizzo Mgunda na Hamma Kinyoya, mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja la Maimuna, mcheza shoo wa kundi hilo, ambaye jina lake halijaweza kujulikana mara moja na mbeba vyombo Haji Mzaniwa.
Waliojeruhiwa katika ajali hiyo na ambao wamelazwa katika hospitali ya mkoa wa Morogoro ni mwimbaji mkongwe na mgeni aliyekuwa amefanya onyesho moja na kundi hilo, Mwanahawa Ally, Suzana Benedict , Zena Mohamed, Samila Rajab, Ally Juma, Rajab Kondo,Mwanahawa Hamis, Shaban Hamis na Msafiri Mussa.
Kwa sababu kifo kimeumbwa na hakuna binadamu anayeweza kukikwepa, napenda kuchukua fursa hii kuwaomba ndugu wa wasanii waliofariki dunia kuwa na moyo wa subira na ustahamilivu.
Ni kawaida unapotokea msiba mkubwa na wa kushtukiza kama huo, baadhi ya watu huzusha maneno mengi, ikiwa ni pamoja na kuvihusisha vifo vya aina hiyo na mambo ya ushirikina. Lakini napenda waamini kuwa huo ni msiba kama mingine na umepangwa na Mungu. Hakuna ambaye angeweza kuukwepa wala kuuzuia.
Ni vyema ndugu wa wasanii waliofariki dunia wakubali kwamba hiyo ni mipango ya Mungu, hakuna anayeweza kuipinga. Wanapaswa kuamini kuwa, duniani tunapita njia, makazi yetu ya kudumu ni ahera.
Wakumbuke kuwa, binadamu sote tunapita katika madaraja matatu. La kwanza ni kuzaliwa, la pili ni kuishi na la tatu ni kifo. Hivyo vyovyote iwavyo, binadamu sote lazima tuonje mauti.
Na kwa wale wasanii waliojeruhiwa, tunawaombea kwa Mola wapate nafuu ili watakapotoka hospitali waweze kuendelea na shughuli zao za kila siku zinazowaendeshea maisha yao. Nao waamini kuwa, ajali hiyo ni mipango ya Mungu kamwe si mkono wa mtu. Ndivyo maisha yalivyo.
Mungu awalaze pema peponi wasanii wote 13 wa Five Stars Modern Taarab waliofariki dunia katika ajali hiyo na awape ahueni wale waliojeruhiwa.

No comments:

Post a Comment