KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, March 10, 2011

BINGWA KOMBE LA NSSF KUPATA Mil 3.5/-

MKURUGENZI wa Uendeshaji wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Crescentius Magori (kushoto) akikabidhi vifaa vya michezo kwa Katibu wa klabu ya Uhuru, Rashid Zahor (kulia) katika hafla iliyofanyika jana makao makuu ya mfuko huo mjini Dar es Salaam. Katikati ni Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya Kombe la NSSF, Masoud Saanani. (Picha kwa hisani ya Francis Dande wa globu ya Jami).

BINGWA wa michuano ya soka ya Kombe la NSSF kwa mwaka 2011, atazawadiwa kitita cha sh. milioni 3.5 wakati mshindi wa netiboli atapata sh. milioni tatu.
Akitangaza zawadi hizo kwa waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Crescentius Magori alisema, mshindi wa pili katika soka atazawadiwa sh. milioni 2.5 na watatu sh. milioni 1.5.
Magori alisema mshindi wa pili wa netiboli atazawadiwa sh. milioni mbili wakati mshindi wa tatu atapata sh. milioni moja. Alizitaja zawadi zingine kuwa ni sh. milioni 2.5 kwa wafungaji wa michuano yote miwili.
Kwa mujibu wa Magori, wameamua kuiboresha zaidi michuano ya mwaka huu kwa kuongeza zawadi kwa washindi, ambapo jumla ya zawadi zote ni sh. milioni 14.
Mkurugenzi huyo alisema NSSF inaona fahari kuandaa michuano hiyo kwa vile imekuwa ikisaidia kutangaza shughuli zake na kuwataka washindi waheshimu kanuni walizojiwekea.
Alisema kamati ya mashindano imejitahidi kuzifanyiakazi dosari zote zilizojitokeza katika michuano iliyopita na kuongeza kuwa, katika siku zijazo, huenda ikazishirikisha timu zingine kutoka nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano hayo, Masoud Saanani alisema, jumla ya timu 17 zinatarajiwa kuchuana katika mchezo wa soka na zingine 11 katika netiboli.
Masoud alivitaja vyombo vya habari vitakavyoshiriki katika michuano ya mwaka huu kuwa ni wenyeji NSSF, Mlimani Media, Changamoto, New Habari, IPP Limited, Global Publishers, Habari Zanzibar, Mwanahalisi na Radio Kheri.
Vingine ni Free Media, Uhuru Publications Ltd, Tumaini Media, Mwananchi, Jambo Leo, Sahara Communications, Business Times na TBC.
Mwenyekiti huyo alisema michuano ya mwaka huu itachezwa kwa mtindo wa ligi, ambapo timu za soka zimegawanywa katika makundi manne, moja likiwa na timu tano na matatu yakiwa na timu nne kila moja.
Alisema kundi A litakuwa na timu za Business Times, Changamoto, NSSF na Mlimani Media wakati kundi B litakuwa na timu za Habari Zanzibar, Global Publishers, New Habari na Radio Kheri.
Kundi C litakuwa na timu za Uhuru, Mwananchi, Mwanahalisi, Tumaini Media na Sahara Communications wakati kundi D litakuwa na timu za IPP, TBC, Jambo Leo na Freee Media.
Kwa upande wa netiboli, Masoud alisema kundi A litakuwa na timu za NSSF, Global Publishers na Tumaini Media, kundi B timu za Mwananchi, Uhuru, New Habari na Free Media wakati kundi C litakuwa na timu za Business Times, Habari Zanzibar, TBC na IPP.
Michuano ya mwaka huu imepangwa kuanza Machi 19 hadi Aprili 16 mwaka huu na itachezwa kwenye viwanja vya TCC na Chuo Kikuu Kishiriki cha Ualimu (DUCE) vilivyopo Chang’ombe, Dar es Salaam.
Katika mechi za ufunguji, mabingwa watetezi wa soka, Business watamenyana na wenyeji NSSF wakati katika netiboli, Global Publishers watamenyana na Tumaini Media.

No comments:

Post a Comment