BAADHI ya wanachama wa klabu ya Yanga, Jumanne iliyopita walinusurika kuchapana makonde kwenye makao makuu ya klabu hiyo, kufuatia baadhi yao kuandaa mkutano wa matawi bila ya kuwashirikisha viongozi wa klabu hiyo.
Tukio hilo lilitokea saa tisa alasiri baada ya baadhi ya viongozi wa matawi kupanga kumuondoa madarakani Mwenyekiti wa matawi ya klabu hiyo nchini, Mohamed Msumi.
Kundi la wanachama la Yanga Bomba lilifika kwenye makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya mkutano huo wa kumjadili Msumi.
Mara baada ya kufika kwenye klabu hiyo, kundi hilo likiwa na baadhi ya viongozi wa matawi, lilishindwa kufanya mkutano wake baada ya kuwakuta wanachama wengine wanaomuunga mkono Msumi wakilinda usalama wa klabu.
Kufuatia hali hiyo, yalitokea mabishano makali kati yao na kusababisha baadhi ya wanachama kutaka kupigana, kufuatia kila ipande kudai kuwa, una haki. Hali hiyo ilisababisha Kaimu Katibu Mkuu wa klabu hiyo ,Mwesingwa Joas Selestin kueleza kuwa hakuwa na taarifa ya mkutano huo.
Mwesingwa alilazimika kuondoka haraka kwenye majengo ya klabu hiyo kwa kutumia mlango wa nyuma ili kukwepa vurugu hizo huku baadhi ya wanachama wakisikika wakieleza kuwa, wataharibu vifaa vya jengo hilo.
Uchunguzi uliofanywa na Burudani umebaini kuwa, fujo hizo zilitokea baada ya baadhi ya wanachama kutaka Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Davis Mosha arejeshwe madarakani huku wengine wakipinga.
Mosha aliandika barua ya kujiuzulu uongozi wa klabu hiyo hivi karibuni na kusababisha hali ndani ya klabu hiyo kuchafuka baada ya kutishiwa kuuawa huku gari lake likivunjwa kioo cha nyuma.
Gari la kiongozi huyo lilivunjwa kioo hicho mara baada ya mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara kati ya Yanga na Polisi ya Dodoma uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Hali imezidi kuchafuka ndani ya Yanga kufuatia baadhi ya wanachama kudai kwamba, klabu hiyo imekuwa ikikosa mapato makubwa ya mauzo ya jezi na vitu vyenye nembo ya Yanga.
Wanachama hao wanawashutumu baadhi ya viongozi wao kuwa wanahusika na uchapishaji wa fulana, kalenda na vitu vingine kwa kutumia nembo ya klabu na kisha kuviuza.
Alipoulizwa kuhusu vurugu zilizotokea Jumanne iliyopita, Mwenyekiti wa matawi ya klabu hiyo, Msumi alikiri kutokea kwake, lakini alisema hakuwa na taarifa za kuwepo kwa mkutano wa wanachama.
No comments:
Post a Comment