'
Thursday, March 17, 2011
Sikinde, Msondo Ngoma kazi ipo kesho
BENDI kongwe za muziki wa dansi nchini, Msondo Ngoma na Mlimani Park Orchestra kesho zinatarajiwa kuonyeshana ubabe katika onyesho litakalofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Onyesho hilo la kihistoria limeandaliwa na Kampuni ya Prime Time Promotions kwa lengo la kuonyesha uhai wa bendi hizo na pia kuwapa mashabiki burudani kabambe.
Taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo jana imeeleza kuwa, onyesho hilo limepangwa kuanza saa nne usiku na kiingilio ni sh. 5,000 kwa mtu mmoja.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bendi hizo zitapanda jukwaani kwa awamu na kupiga nyimbo zao mpya na za zamani kwa lengo la kuwapa mashabiki ladha tofauti ya muziki.
Hii ni mara ya pili katika kipindi cha miezi mitano kwa bendi hizo mbili kufanya onyesho la pamoja. Mara ya mwisho zilionyeshana kazi mwishoni mwa mwaka jana kwenye ukumbi wa Mzalendo Pub, Kijitonyama, Dar es Salaam.
Akizungumzia onyesho hilo, Katibu wa Mlimani Park, Hamisi Milambo alisema wamejiandaa vyema kuwadhihirishia mashabiki wao kwamba wao ni mabingwa halisi wa muziki nchini.
Alisema kukosekana kwa mwimbaji wao nyota, Shaban Dede aliyejiunga na Msondo Ngoma juzi hakuwezi kuwaathiri kwa vile bendi yao ina hazina ya waimbaji wengi wazuri.
“Tumekuwepo kambini kwa takriban wiki moja tukizifanyia mazoezi nyimbo zetu za zamani kwa lengo la kuwakumbusha mashabiki tulipotoka, tulipo na tunapokwenda,”alisema.
Aliwataja waimbaji wengine watakaopanda jukwaani siku hiyo kuwa ni Hassan Bitchuka, Hassan Kunyata, Abdalla Hemba na wapiga ala kama vile Ramadhani Mapesa, Karama Tony na Steven Maufi.
Naye Meneja wa Msondo Ngoma, Saidi Kibiriti alisema, hawana wasiwasi na onyesho hilo kwa vile wamefanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya kuwasambaratisha wapinzani wao.
Alisema kuongezeka kwa Dede kwenye kikosi chao kutaiongezea nguvu bendi hiyo kwa vile wamemchukua kwa lengo la kuziba mapengo ya waimbaji mbalimbali, ambao kwa sasa hawapo.
Kibiriti amewataka mashabiki wa Msondo Ngoma kujitokeza kwa wingi kuhudhuria onyesho hilo kwa lengo la kuwaongezea ari na nguvu ya kufanya vizuri.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment