Na Emmanuel Ndege
MSHAMBULIAJI wa zamani wa klabu ya Yanga, Bernard Mwalala ametua nchini kwa ajili ya kufanya mazungumzo na Kocha Sam Timbe.
Mwalala alitua nchini wiki iliyopita kwa ajili ya kufanyiwa majaribio na Timbe ili aweze kuichezea tena Yanga msimu ujao.
Mshambuliaji huyo aliyeichezea Yanga kwa mafanikio makubwa, alikuwepo uwanjani wakati timu hiyo ilipomenyana na mahasimu wao Simba katika mechi ya ligi na kutoka sare ya bao 1-1.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam wiki hii, Mwalala alisema amekuja nchini kwa ajili ya kukutana na Timbe ili kuangalia kama anaweza kumfanyia majaribio.
"Napenda kujiunga tena na Yanga. Nilikuwa Uganda kwa siku chake pale SC Villa, sasa nataka kurejea kuitumikia klabu hii, ambayo naipenda toka moyoni mwangu,"alisema mchezaji huyo ambaye ni raia wa Kenya.
Mmoja kati ya viongozi wa benchi la ufundi la timu hiyo, ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, alisema mchezaji huyo ameshafanya mazungumzo na Timbe.
Mchezaji huyo pia amekuwa akifika kwenye mazoezi ya Yanga mara kwa mara yanayofanyika katika uwanja wa Uhuru huku akionyesha kuvutiwa na wachezaji waliopo kwenye kikosi hicho.
Akizungumzia ujio wa mchezaji huyo, Timbe alisema anamfahamu vizuri Mwalala na ana imani ataweza kuisaidia timu hiyo katika msimu ujao wa ligi kuu.
Hata hivyo, Timbe alisema atalazimika kumfanyia majaribio mchezaji huyo kabla ya kuamua kumsajili au la.
No comments:
Post a Comment