KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, March 1, 2012

Taifa Stars yawakera watanzania









LICHA timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kucheza nyumbani mbele ya maelfu ya mashabiki wake ilishindwa kuwapa raha, baada ya jana kutoshana nguvu na Msumbiji 'Black Mambas' katika mechi ya kuwania tiketi ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika.

Timu hizo zilitoka sare ya kufungana bao 1-1 katika mechi, ambayo imeharibu taswira ya Stars kujitengenezea mapema mazingira mazuri ya kucheza fainali hizo mwakani nchini Afrika Kusini.

Stars wakicheza katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, walimnyima raha kocha Jan Poulsen aliyeshindwa kukaa kwenye benchi na muda wote alikuwa anatoa maelekezo kwa wachezaji kana kwamba, hakufanya hivyo kwenye mazoezi ya kujiandaa na mechi hiyo.

Pamoja na kocha huyo kujaza viungo wengi walioongezewa nguvu na Nizar Khalfan, ambaye alitolewa baada ya kushindwa kuhimili presha ya mamba hao na hivyo nafasi yake kuingizwa Ngassa, ambaye pia hakuongeza 'chaji' kwa timu hiyo na kuishia kulazimisha sare hiyo.

Kiungo mshambuliaji Abdi Kassim 'Babi' ndiye aliyeigharimu Taifa Stars, baada ya kupokwa mpira na Clesio Bauque, ambaye aliwatoka mabeki watatu wa timu hiyo na kupiga mkwaju uliomshinda kipa Juma Kaseja.

Viungo wa Stars waliisumbua ngome ya Msumbiji na juhudi zao zilizaa matunda dakika 42 baada ya Kazimoto kufunga bao la kusawazisha kwa shuti la mbali akiunganisha krosi ya Vicent Barnabas.

Hadithi za timu hiyo kuishindwa Msumbiji kwa kucheza nayo mara tatu katika uwanja huo wa taifa na kuishia kufungwa mara moja na sare hiyo huku wakipigwa na mamba hao. Aprili mwaka jana katika mchezo wa ufunguzi wa uwanja mjini Maputo, ziliendelea kwa mshambuliaji John Bocco kushindwa kuweka kimiani pasi ya Babi.

Bocco ni sehemu ya wachezaji walioshindwa kuonyesha umuhimu wake katika mchezo huo kwa kupoteza nafasi nne za wazi, huku mashabiki wakishindwa kuamini kinachotokea uwanjani.

Kosakosa iliendelea kwa Kazimoto kuitoka ngome ya Msumbiji dakika 34 na kupiga mpira wa krosi uliokolewa na mabeki wa Msumbiji wanaokwenda kuisubiri Taifa Stars nyumbani kwao wakiwa na mtaji wa bao la ugenini.

Bauque alimjaribu Kaseja kwa shuti dakika 38 lililopanguliwa na kipa huyo. Dakika 45 za mwanzo, Stars ilicheza vyema huku Barnabas na Kazimoto wakitoa mchango mkubwa katika nafasi zao.

Taifa Stars: Juma Kaseja, Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika, Juma Nyoso, Aggrey Morris, Shaaban Nditi, Nizar Khalfan/Ngasa, Mwinyi Kazimoto, John Bocco, Abdi Kassim na Vincent Barnabas.

Msumbiji: Joao Raphael, Edson Sitoe, Zainadine Junior, Eduardo Jumisse, Jerenias Sitoe, Elias Pelembe, Clesio Bauque, Francisco Muchanga, Stelio Erneso, Francisco Massinga na Almiro Lobo.

No comments:

Post a Comment