KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 2, 2012

HATIMAYE NGASA AMWAGA WINO SIMBA, ALIPWA MIL 35/- NA GARI

HAKUNA utata tena. Tamka Mrisho Khalfan Ngassa ni mchezaji halali wa Simba SC. Mchana huu, klabu ya Simba imefanikiwa kumalizana na Ngassa na kusaini naye mkataba wa miaka miwili, ambao umemfanya aondoke na zaidi ya Sh. Milioni 35, Milioni 12 akipewa taslimu na nyingine akipewa gari.
Katika mkataba huo wa Simba na Ngassa, mshambuliaji huyo atakuwa akilipwa Sh. Milioni 2 mshahara kwa mwezi, Milioni 1 ipo kwenye mkataba na Milioni 1 atakuwa akiongezewa na mtu. Nani kakamilisha dili hili? Ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Hans Pop ndiye katoa fedha hizo na baada ya kumsainisha na kumkabidhi haki yake, ili kumuondolea usumbufu akambadilishia ‘chipu’ ya simu, ili akina Seif Magari wasimpate.

Jana Simba ilimnunua Ngassa kutoka Azam kwa Sh. Milioni 25, lakini mchezaji huyo wa zamani wa Yanga akagoma kwa sababu hakushirikishwa katika dili hilo. Leo asubuhi Ngassa alizungumza na Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji, Alex Mgongolwa kupinga kuuzwa kwake katika klabu hiyo, akitokea Azam FC bila kuhusishwa.

Akizungumza na BIN ZUBEIRY asubuhi ya leo, Ngassa alisema kwamba hajafanya mazungumzo na Simba SC wala Azam FC juu ya uhamisho. “Mimi sijui chochote, na sikatai kuhamishwa, kwa sababu mimi soka ni kazi yangu na ninaweza kucheza popote, ila taratibu zifuatwe tu,”alisema.

Ngassa alisema baada ya kuona mambo yanakwenda kinyume cha utaratibu, aakaamua kulifikisha suala lake Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ili haki itendeke.

Kwa hatua hiyo, Simba imeamua kuzungumza naye na kumaliza naye na sasa kijana ataanza mazoezi Simba wiki ijayo, akitoka Mwanza anakokwenda leo kusalimia wazazi.

Azam ilifikia uamuzi wa kumuuza Ngassa, baada ya mchezaji huyo iliyemsajili kutoka Yanga miaka miwili iliyopita, kubusu jezi ya Yanga baada ya kufunga bao la pili katika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Na uamuzi huo, ni wa mzee Said Salim Bakhresa mwenyewe, ambaye alikerwa na kitendo hicho akawaagiza wanawe, Wakurugenzi wa bodi ya timu wamuuze mchezaji huyo popote, haraka iwezekanavyo.Ngassa alikuwa amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake aliosaini na Azam FC, akitokea Yanga miaka miwili iliyoipita kwa dau la Sh. Milioni 55, lakini wasiwasi unakuja kwamba, Ngassa ana mapenzi na Yanga na kwa Simba kumsajili, kuna hatari yaliyotokea akiwa Azam, yatajirudia hata akiwa kwa Wekundu wa Msimbazi.

Mapema jana mchana, Stewart Hall, kocha Muingereza wa Azam FC jana alifukuzwa katika klabu hiyo kwa kosa la kukaidi maagizo ya Bodi ya Ukurugenzi ya klabu hiyo, kumpanga Mrisho katika mechi ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.

Habari ambazo BIN ZUBEIRY ilizipata kutoka ndani ya Azam, zilisema kwamba kikao cha jana cha pamoja baina ya Bodi ya Ukurugenzi ya Azam FC, Mwanasheria wa kampuni na kocha Stewart kimeafiki kuvunja ndoa hiyo na sasa Azam FC itakuwa chini ya kocha kutoka India, Vivek Nagul ambaye alikuwa anafundisha timu ya vijana.

Habari zinasema kwamba, mapema baada ya mechi ya Nusu Fainali ya Kagame, kati ya Azam na AS Vita ya DRC, Stewart aliitwa na kuambiwa asimtumie tena Ngassa kwa kitendo cha mchezaji huyo kwenda kuibusu na kuivaa jezi ya Yanga, baada ya kufunga bao la ushindi.

Lakini Stewart katika kikao hicho, kwanza alimtetea Ngassa kutokana na kufunga bao la ushindi na kumuelezea kama mchezaji muhimu kwake, lakini msimamo wa bodi ulikuwa ni asipangwe tena.

Katika fainali, Stewart alimvalisha jezi Ngassa akamuanzishia benchi, lakini kama ilivyokuwa kwenye Nusu Fainali alimuingiza kipindi cha pili timu ikiwa nyuma kwa 1-0 na mwisho wa mchezo ikashinda 2-1 yeye akifunga la pili, dhidi ya Yanga pia alimuingiza timu ikiwa nyuma kwa 1-0.

Lakini Ngassa alishindwa kurudia kile alichofanya kwenye mechi na AS Vita na Yanga ikashinda 2-0.Kwa kutua Simba, Ngassa amefuata nyayo za baba yake mzazi Khalfan Ngassa ambaye alichezea klabu hiyo kati ya 1990 hadi 1992.

CHANZO CHA HABARI; BIN ZUBEIRY

No comments:

Post a Comment