KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 9, 2012

'TUMIENI KISWAHILI KWENYE FILAMU ZENU'

SERIKALI imewataka wasanii wa filamu nchini kutumia lugha ya kiswahili kwenye filamu zao kwa lengo la kulinda na kutukuza utamaduni wa Mtanzania.
Mwito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Profesa John Nkoma mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akifungua semina iliyoandaliwa na Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) mjini Dar es Salaam.
Profesa Nkoma aliwapongeza wasanii wa fani hiyo kwa kuanzisha chombo chao, ambacho lengo lake kubwa ni kuwaunganisha, lakini aliwasihi kuiheshimu na kuitukuza lugha ya kiswahili kwenye filamu zao.
“Ukitazama filamu kutoka Bollywood, unaona kabisa utamaduni wao, lakini hata ndugu zetu wanigeria kupitia filamu zao, unaona utamaduni wao, lakini hapa kwetu, kuna watu wanawaiga wanigeria katika uzungumzaji wao,”alisema.
Mkurugenzi huyo wa TCRA alisema kuiga utamaduni wa kigeni si jambo zuri kwa sababu kunaweza kusababisha kazi za kitanzania zikapoteza mvuto.
Alisema ni vyema kwa wasanii wa filamu nchini kutengeneza kazi zao zikiwa na mwelekeo wa utamaduni wa mtanzania badala ya kuutangaza na kuutukuza utamaduni wa kigeni.
Profesa Nkoma alisema anapenda kuwaona wasanii wa filamu wa Tanzania wakipiga hatua kubwa kimaendeleo kama ilivyo kwa wasanii wa Nigeria.
“Kila jambo ukijipanga, linawezekana na kufanikiwa, hata sisi awali tuliposema tunataka kujenga jengo kubwa, ambalo ndimo mlimo leo hii mkifanyia mkutano huu, watu walibeza kwa kusema hatutaweza, lakini leo hii jengo limekamilika na linatumika,”alisema Prof. Nkomo.
Semina hiyo iliandaliwa na TAFF na kudhaminiwa na TCRA, ilifanyika kwa siku mbili na kuhudhuriwana wadau mbali mbali wa filamu. Wawezeshaji wa semina hiyo walitoka taasisi ya Tanzania Consultech International Limited wakati mtoa mada mkuu alikuwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Profesa Elisante Ole Gabriel.

No comments:

Post a Comment