MWIMBAJI nyota wa zamani wa bendi za muziki wa dansi za African Revolution na Double M Sound, Amina Ngaluma amezikwa.
Mazishi ya mwanamuziki huyo yalifanyika jana katika makaburi ya Machimbo Mnarani, Kitunda, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi.
Amina alifariki dunia wiki iliyopita nchini Thailand baada ya kuugua kwa muda mfupi na mwili wake ulirejeshwa nchini Ijumaa iliyopita kwa ndege.
Mwanamuziki huyo alikuwepo Thailand kwa zaidi ya miaka miwili, akipiga muziki katika bendi ya Jambo Survivors.
Baadhi ya wanamuziki wakongwe na chipukizi ni miongoni mwa mamia ya watu waliojitokeza kumsindikiza mwanadada huyo katika safari yake ya mwisho duniani.
Miongoni mwa wanamuziki wakongwe waliohudhuria mazishi hayo ni John Kitime, Cosmas Chidumule, Waziri Ally, Ally Choki, Muumin Mwinjuma, Abdalla Mgonahazelu, Rogert Hegga na Super Nyamwela.
Wakizungumza na blogu hii wakati wa mazishi hayo, baadhi ya wanamuziki walikielezea kifo cha Amina kuwa ni pigo kubwa katika tasnia hiyo kutokana na uhodari wake wa kutunga na kuimba nyimbo zenye mvuto.
No comments:
Post a Comment