MWANACHAMA maarufu wa klabu ya Simba, Evans Aveva (kulia) amechukua fomu ya kuwania uenyekiti
UCHAGUZI Mkuu wa klabu ya Simba umeanza kupamba moto baada ya katibu mkuu msaidizi na mjumbe wa zamani wa kamati ya utendaji, Evans Aveva kuchukua fomu ya kuwania uenyekiti.
Aveva alichukua fomu jana asubuhi makao makuu ya klabu hiyo mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam, akiwa amesindikizwa na msafara wa wanachama wa klabu hiyo.
Msafara huo uliongozwa na wanachama waliokuwa wakiendesha pikipiki huku wengine wakiwa wamejazana kwenye mabasi mawili aina ya double coaster.
Baada ya kuchukua fomu, msafara huo wa Aveva uliondoka klabuni hapo na kurudi tena saa 8.45, ambapo mgombea huyo alirejesha fomu yake.
Aveva amekuwa mwanachama wa kwanza kujitokea kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu wa Simba, unaotarajiwa kufanyika Juni 29 mwaka huu.
Wagombea wengine wanaotarajiwa kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo ni pamoja na Katibu Mkuu wa zamani wa klabu hiyo, Michael Wambura.
Uchunguzi wa blogu hii umebaini kuwa, Wambura na Aveva ndio wanaoungwa mkono na wanachama wengi katika kuwania nafasi hiyo inayoshikiliwa na Ismail Aden Rage.
Mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, Hassan Dalali naye ametajwa kuwa miongoni mwa wagombea wanaotarajiwa kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo, japokuwa haungwi mkono na wanachama wengi kama ilivyokuwa zamani.
Mwanachama mwingine aliyechukua fomu hadi sasa ni Alfred Elia, anayewania nafasi ya mjumbe wa kamati ya utendaji. Mwisho wa kuchukua na kurejesha fomu ni Jumanne.
Nafasi zinazogombewa katika uchaguzi huo ni ya mwenyekiti, makamu mwenyekiti na ujumbe wa kamati ya utendaji.
No comments:
Post a Comment