'
Tuesday, May 20, 2014
MWILI WA AMINA NGALUMA KUREJESHWA DAR IJUMAA
MWILI wa mwimbaji mahiri nchini aliyefariki dunia wiki iliyopita nchini Thailand, Amina Ngaluma ‘Japanese’ unatarajiwa kuwasili Dar es Salaam Ijumaa wiki hii.
Kwa mujibu wa mume wa marehemu, Rashid Sumuni tayari taratibu muhimu kuhusiana na kuuleta mwili huo nyumbani zimefanyika na wana amini mambo yataenda kama wanavyotarajia.
“Naomba niwajulishe kuwa mwili wa mke wangu utaondoka Thailand Alhamisi wiki hii kwa ndege ya KLM na utawasili Dar es Salaam siku inayofuata saa tatu usiku.
“Tunaamini kama mambo yataenda kama tulivyopanga baada ya mwili kuwasili basi Jumamosi tutamhifadhi mwenzetu. Msiba upo kwa wazazi wa marehemu Kitunda, Machimbo, Dar es Salaam ambako ndiko maziko yatafanyika.
“Kimsingi imekuwa ngumu kusema tutazika lini, kwa sababu bado mwili haujaletwa, lakini tayari familia kwa kushirikiana na sehemu alikokuwa anafanya kazi na Watanzania wengine waishio kule tumeshamaliza taratibu zote zilizokuwa zikihitajika ili kuuleta mwili nchini,” alisema Sumuni kwa masikitiko.
Pia alivishukuru vyombo vya habari kwa kuwa karibu na familia yao wakati wa kipindi hiki kigumu, lakini akiomba wanapotaka kutoa habari kuhusiana na msiba huo wawasiliane na wahusika wa familia ili kupata taarifa sahihi zaidi.
Ngaluma aliyepata kung’ara na bendi mbalimbali nchini, alifariki dunia Alhamisi iliyopita kwa shinikizo la damu akiwa Thailand alikokuwa akifanya shughuli za muziki katika bendi ya Jambo Survivor.
Wakati wa uhai wake alitamba na bendi mbalimbali zikiwemo African Revolution ‘Tamtam’, Double M Sound ‘Mshikemshike’ na TOT Plus zote za Dar es Salaam.
Pia alipigia makundi ya Arusha Sangoma, Sayari Band na Less Mwenge yote ya Arusha na Mangelepa na Sky Sound za Kenya. Pia amepata kufanya shughuli za muziki kwa miezi sita nchini Uganda.
Baadhi ya nyimbo alizotunga wakati wa uhai wake ni Manyanyaso Kazini na Mapendo alizotunga akiwa Tamtam, wakati Double M Sound alitunga nyimbo za Wajane na Ukewenza.
Pia alitoa albamu yake binafsi iitwayo Jitulize yenye nyimbo kama Vidonge, Pete ya Uchumba, Good Night, Uombalo Hutopata, Jitulize na Mzigo wa Moto.
Baadhi ya nyimbo alizopata kuimba na kumpatia umaarufu mkubwa ni Mgumba, Maisha Kitendawili, Ndugu Lawama, Zawadi ya Watanzania, Ugumu wa Maisha na Call Box zote zikitungwa na Muumin Mwinjuma ‘Kocha wa Dunia’.
Shiwata yawalilia Amina na Kuambiana
MTANDAO wa Wasanii Tanzania (SHIWATA)umepokea kwa majonzi kifo cha mwanamuziki mashuhuri na maarufu wa mwanamuziki wa dansi nchini,Amina Ngaluma "Japanese" aliyefariki nchini Thailand.
Marehemu Ngaluma aliyekuwa mwanachama wa SHIWATA atakumbukwa kwa mengi mazuri aliyoyafanya akiwa mwanamuziki wa kike mwenye kipaji cha kutunga,kuimba na kutawala jukwaa katika maonesho ya akiwa na bendi mbalimbali ikiwemo Tam Tam, Double M,Tanzania One Theatre (TOT).
Ngaluma pia amewahi kufanya maonesho katika bendi za nje ya nchi kama Kenya na Thailand ambako amepatwa na mauti akiwa akifanya maonesho katika moja ya hoteli za kitalii.
SHIWATA inachukua nafasi hii kutoa pole familia ya Mzee Ngaluma kwa kuondokewa na mtoto wao mpendwa ambaye mbali ya mchango wake ulisaidia familia yake lakini pia taifa limepata pengo kwani alitumia kipaji chake cha sanaa kuelimisha, kuburudisha na kuitangaza Tanzania ndani na nje ya nchi.
Mtandao pia unaungana na familia ya msanii wa Bongo Movie, Adam Kuambiana katika msiba uliomkuta juzi wakati mchango wake bado unahitajika katika fani hiyo.
Mchango wa Kuambiana umeacha pengo kubwa katika tasnia ya filamu nchini Tanzania kwa uwezo mkubwa aliokuwa nao wa kuigiza na kuongoza filamu alizowahi kucheza kama ya Salt.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment