KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, May 6, 2014

UWANJA WA SOKOINE MBEYA KUWEKWA NYASI BANDIA



NA SOLOMON MWANSELE,MBEYA.


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), linatarajia kutuma wawakilishi kutoka CAF na FIFA ili kuufanyia ukaguzi uwanja wa Sokoine, kuona kama una vigezo vya kuweza kutumika kwa mashindano ya michezo ya kimataifa.

Imeelezwa wataalamu hao kutoka CAF na FIFA wanatarajiwa kuwasili jijini Mbeya, hivi karibuni kwa ajili ya kufanikisha ukaguzi huo.

Rais wa TFF,Jamal Malinzi, aliyasema hayo jana alipokuwa akijibu maswali mbalimbali ya waandishi wa habari,mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya Malawi na Taifa Stars, uliochezwa uwanja wa Sokoine,mjini hapa.

Malinzi alisema lengo la TFF ni kuhakikisha kuwa michezo ya ngazi za kimataifa inachezwa katika viwanja mbalimbali nchini na siyo kuishia Dar es Salaama pekee yake.

Alisema wataalamu hao kutoka CAF na FIFA watafika uwanja wa Sokoine kwa ajili ya kuukagua ili kuweza kuona kama unafaa na unastahili kwa mechi za kimataifa na hilo likipita wapenzi wa soka Mbeya wategemee kuona mechi nyingi za kimataifa.

Aliongeza hivi sasa Shirikisho hilo linahangaika kuhakikisha kuwa viwanja vya michezo katika mikoa mingine nchini vikiwemo Nelson Mandela, kilichopo Sumbawanga, nacho kinaboreshwa ili michezo ya kimataifa iweze kupelekwa huko.

“Uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo jijini Arusha, CCM Kirumba uliopo Mwanza tunataka kuhakikisha kama uwanja unakidhi hadhi basi michezo ya kimataifa inapelekwa ili kutoa burudani kwa watanzania wengi zaidi” alisema Malinzi.

Kuhusu Taifa Stars, Rais huyo wa TFF alisema wamempata Kocha mpya,Mart Nooij kutoka nchini Uholanzi,ambaye ni mtaalamu aliyekaa na wachezaji kambini kwa muda mfupi na pia ameuona mchezo na Malawi maarufu zaidi The Flames.

Kwa mujibu wa Malinzi, bila shaka Kocha Nooij baada ya kukiona kikosi hicho kikicheza ataona yeye kama kuna mabadiriko anataka kuyafanya na ini imani ya TFF kufika Mei 18, mwaka huu timu itakapocheza na Zimbabwe iitakuwa imebadirika zaidi.

Malinzi alisema lakini wapenzi wa soka wameweza kuona jinsi timu hiyo inavyocheza kitimu zaidi, kwani licha ya kutoibuka na ushindi katika mchezo huo lakini imeweza kufika golini mwa Malawi na kukosa magoli ya wazi manne.

“Mmemuona mshambuliaji wetu John Bocco amekosa magoli mawili, na mawili mengine likiwemo la kichwa la Aggrey Morris…Lakini yote haya ni jambo la kawaida kwenye mchezo wa soka” alisema Malinzi.

Kikubwa zaidi katika mchezo huu, ni kuwa tumeshambuliwa na Malawi lakini bado tumeweza kuzuia vizuri na hatujafungwa goli,kwani ni lazima uangalie kama umefika kwa adui na adui alipokushambulia umefanya nini.

Rais wa TFF aliongeza hivi sasa beki ya Taifa Stars, wachezaji wa viungo na hata washambuliaji wameimarika zaidi kwa kuweza kufanya mashambulizi mengi langoni mwa Malawi.

No comments:

Post a Comment