MBIO za uchaguzi mkuu wa Simba zinatarajia kuanza rasmi wakati wowote kuanzia sasa, baada ya marekebisho ya katiba ya klabu hiyo kupitishwa rasmi.
Katiba hiyo imepitishwa na ofisi ya Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo nchini, ambapo uongozi wa Simba kesho utatangaza tarehe ya uchaguzi mkuu wa klabu hiyo.
Msajili ameipitisha katiba hiyo lakini amekataa kipengele kilichofanyiwa marekebisho na wanachama wa Simba cha kutaka mwanachama aliyewahi kufungwa kwa kosa la jinai, aruhusiwe kugombea.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema leo Kamati ya Uchaguzi chini ya Mwenyekiti Damas Ndumbaro na makamu wake Salum Madenge, itakutana kwa ajili ya kupanga tarehe ya uchaguzi.
"Uchaguzi wa Simba sasa umeiva niwaombe tu wanachama watumie fursa yao kuhakikisha wanachangamkia nafasi za uongozi," alisema Kamwaga.
Alisema kilichokuwa kikisubiriwa kilikuwa ni katiba na kwa kuwa imeshapatikana, hakuna kipingamizi cha uchaguzi huo.
Kamwaga alisema katika mapendekezo yote yaliyomo kwenye katiba hiyo yaliyoazimiwa katika mkutano mkuu wa wanachama uliofanyika Machi 16 mwaka huu, yamepitishwa isipokuwa kimoja cha sifa ya mgombea.
Alisema pia kwa mujibu wa katiba hiyo mpya ya Simba, nafasi ya mwenyekiti sasa itajulikana kama Rais na nafasi ya makamu imebadilika na kuwa Makamu wa Rais.
Katibu huyo katiba ya Simba imepitisha sheria mpya ambayo inataka tawi la Simba liwe na wanachama wasiozidi 250 katika kila kata na wasiopungua 50 na kwamba mpaka sasa hakuna tawi lolote la klabu hiyo lenye wanachama hai 250.
Kamwaga pia alisema kupitia katiba hiyo kumeundwa Kamati ya Maadili na Kamati ya Rufani na kati ya wajumbe watano wa kuchaguliwa, nafasi moja lazima iwe ya mwanamke, hivyo amewataka wanawake kuomba uongozi katika klabu hiyo.
Uongozi wa Simba unaomaliza muda wake chini ya Ismail Rage uliingia madarakani Mei 9, 2010, ambapo sasa klabu hiyo inaingia katika mchakato wa kupata viongozi wapya wa klabu hiyo.
Wakati huo huo, wachezaji watakaoachwa na klabu ya Simba wanatarajia kutangazwa kesho kwa lengo la kupewa nafasi ya kutafuta timu nyingine mapema.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema Kamati ya Usajili leo itakaa kikao na wachezaji hao ili kufikia makubaliano nao na kuwaacha watafute timu nyingine.
"Masuala yote ya usajili yapo sawa na tunategemea kesho (leo) kukaa na wachezaji kwa ajili ya kuagana na kuwaacha huru," alisema Kamwaga.
Alisema wameamua kuchukua hatua ya kukaa nao kwanza kabla ya kutangaza majina yao ili kuwaondolea presha.
"Wa kwanza kujua kama wanaachwa ni wao wachezaji hatukupenda tutangaze majina yao kabla ya kuzungumza nao," alisema Kamwaga.
Alisema pia wapo baadhi ya wachezaji ambao wameuomba uongozi waachwe huru, ili kuangalia masuala mengine ya maisha.
Katika ripoti ya kocha mkuu wa Simba, Zdravko Logarusic, amependekeza kikosi kipya cha simba kiwe na wachezaji 25 tu.
Kocha huyo ameagiza kila nafasi iwe na wachezaji wawili wa ndani na makipa watatu.
Kwa mujibu wa Kamwaga, kati ya wachezaji waliopendekezwa na kocha huyo waachwe si wote wataoondolewa kwenye kikosi hicho cha Msimbazi.
"Tutaangalia kulingana na nafasi ya mchezaji husika na kuamua wa kuwaacha," alisema Kamwaga.
No comments:
Post a Comment