KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, May 18, 2014

STARS, ZIMBABWE USO KWA USO LEO



Kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij amesema wachezaji wake wako tayari kwa ajili ya mechi ya Kombe la Afrika dhidi ya Zimbabwe (Mighty Warriors) itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo (Mei 16 mwaka huu), Nooij amesema kabla ya kuja Tanzania alikuwa akifuatilia Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), hivyo anawafahamu wachezaji wengi.

Amesema wachezaji wanaounda kikosi chake ni wenye uzoefu na mechi za kimataifa, hivyo wapo tayari kwa ajili ya mechi hiyo, kwani wamepata mechi za kirafiki na mazoezi ya kutosha kwenye kambi iliyokuwa Tukuyu mkoani Mbeya ambapo kulikuwa na utulivu mkubwa.

Nooij amesema ujio wa washambuliaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (RDC) kutaongeza morali ya kikosi chake.

Samata na Ulimwengu watawasili nchini Jumamosi mchana, saa 7.30 mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines wakitokea Khartoum, Sudan ambapo leo (Mei 16 mwaka huu) wanacheza mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Al Hilal ya huko.

Wachezaji waliopo kambini kwa sasa ni Deogratias Munishi, Aishi Manula, Said Moradi, Oscar Joshua, Kelvin Yondani, Erasto Nyoni, Nadir Haroub, Shomari Kapombe, Aggrey Morris, Himid Mao, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Amri Kiemba, Jonas Mkude, Haruna Chanongo, Simon Msuva, Mrisho Ngasa, Khamis Mcha, Ramadhan Singano, John Bocco, Elias maguli na Kelvin Friday.

Wakati huo huo, timu ya Zimbabwe (Mighty Warriors) inawasili kesho alfajiri (Mei 17 mwaka huu) kwa ndege ya Ethiopian Airlines ikiwa na msafara wa watu 27. Kesho saa 4 asubuhi (Mei 17 mwaka huu) Kocha wa timu hiyo atakuwa na mkutano na waandishi wa habari katika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Tiketi kwa ajili ya mechi hiyo zinaanza kuuzwa kesho (Mei 17 mwaka huu) kwenye vituo vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, mgahawa wa Steers uliopo Mtaa wa Ohio na Samora, OilCom Ubungo, Uwanja wa Taifa, kituo cha mafuta Buguruni na Dar Live Mbagala. Viingilio ni sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 20,000 tu.

MDAU AAHIDI WACHEZAJI MIL 5/-
Mdau mmoja wa mpira wa miguu ambaye hataki jina lake litajwe ameahidi kutoa sh. milioni tano kwa wachezaji wa Taifa Stars iwapo wataifunga Zimbabwe katika mechi ya Jumapili.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linamshukuru mdau huyo, na linatoa mwito kwa wadau wengine wajitokeze kutoa motisha kwa Taifa Stars.

Bonasi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa wachezaji wa Taifa Stars itatolewa kwa mujibu wa taratibu zilizopo.

TFF YAOMBOLEZA VIFO VYA WASHABIKI DR CONGO
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amemtumia salamu za rambirambi mwenzake wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- FECOFA, Omar Constant kutokana na vifo vya washabiki.

Washabiki 12 walipoteza maisha uwanjani wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya nchi hiyo kati ya TP Mazembe na AS Vita iliyochezwa kwenye Uwanja wa Tata Raphael, jijini Kinshasa.

“Tumeguswa na msiba huo mzito, tunatoa salamu za rambirambi kwako (Rais wa FECOFA), familia za marehemu pamoja na wadau wote wa mpira wa miguu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo,” imesema sehemu ya barua hiyo ya Rais Malinzi.

KOZI ZA UKOCHA LESENI A, B KUFANYIKA JUNI
Kocha a ukocha wa mpira wa miguu kwa ajili ya leseni A na B zinazotambuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) zitafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Juni 2 mwaka huu.

Ada kwa kozi zote ni sh. 300,000 ambapo wale watakaofanya ya A (equivalent) itaanza Julai 21-26 mwaka huu. Washiriki wa kozi hiyo ni wale wenye leseni B za ukocha za CAF.

Kwa wale watakaoshiriki kozi ya leseni B ambao ni wale wenye leseni C watakuwa na vipindi viwili. Kipindi cha kwanza ni kuanzia Juni 2-15 mwaka huu wakati cha pili kinaanza Juni 23 mwaka huu na kumalizika Juni 28 mwaka huu.

Wakufunzi wanaotambuliwa na CAF watakaoendesha kozi hiyo ni Sunday Kayuni na Salum Madadi kutoka Tanzania, na washiriki watajigharamia kwa kila kitu. Baadaye CAF watatuma Mkufunzi mwingine kwa ajili ya mitihani.

ULIMWENGU, SAMATA WAJIUNGA STARS
Wachezaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wametua Dar es Salaam leo (Mei 17 mwaka huu) mchana, na kujiunga moja kwa moja kwenye kambi ya Taifa Stars kwa ajili ya michuano ya Afrika dhidi ya Zimbabwe (Mighty Warriors).

Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza ya michuano hiyo itafanyika kesho (Mei 18 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Washambuliaji hao wa Taifa Stars wamewasili saa 7.25 mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines wakitokea Khartoum, Sudan ambapo jana (Mei 16 mwaka huu) timu yao ya TP Mazembe ilicheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal ya huko.

Kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij amesema kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya mechi hiyo, kwani kimepata mechi za kirafiki na mazoezi ya kutosha kwenye kambi iliyoanzia Tukuyu mkoani Mbeya ambapo kulikuwa na utulivu mkubwa.

Naye Kocha Msaidizi wa Zimbabwe, Kalisto Pasuwa amesema hawaifahamu vizuri Taifa Stars lakini wamekuja kwenye mechi hiyo itakayoanza saa 10 jioni kwa ajili ya kushinda, na kuwataka washabiki wajitokeze kwa wingi kuona kiwango cha timu yake.

Milango kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezeshwa na waamuzi kutoka Ghana wakiongozwa na Joseph Odartei Lamptey itakuwa wazi kuanzia saa 6 kamili mchana, na tiketi zitapatikana katika magari maalumu uwanjani hapo.

Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, kijani na bluu, sh. 10,000 kwa VIP C na B, na sh. 20,000 kwa VIP A.

No comments:

Post a Comment