'
Thursday, January 12, 2012
Aki, Ukwa sasa kutoa filamu zao
LAGOS, Nigeria
WACHEZA filamu machachari wa Nigeria, Chinedu Ikedieze ‘Aki’ na Osita Iheme ‘Ukwa’ wanajiandaa kutengeneza filamu mpya kupitia kampuni yao binafsi.
Aki alisema mjini hapa wiki hii kuwa, filamu hiyo itakayogharimu mamilioni ya pesa, itaandaliwa kwa kutumia lugha ya Igbo.
Alisema uamuzi wao huo umelenga kuiokoa lugha hiyo isipotee na pia kuimarisha uhusiano kati yao.
Aki na Ukwa wamekuwa wakishiriki kucheza filamu mbalimbali pamoja na pia kuwa na uhusiano wa karibu kiasi cha kupachikwa jina la mapacha.
“Nilishaahidi mimi binafsi kwamba, nitaandaa filamu tatu kupitia kampuni yangu binafsi ya Chinedu Ikidieze Productions na mbali na hilo, tunayo kampuni yetu ya Aki and Pawpaw Entertainment Nigeria Limited,”alisema Aki.
“Kwa sasa, tupo katika mpango maalumu wa kuandaa filamu kwa lugha ya Igbo, tumeshaandaa filamu kama tatu, ambazo zipo tayari,”aliongeza msanii huyo, aliyefunga ndoa hivi karibuni na mchumba wake wa muda mrefu, Nneoma.
Aki alisema wapo tayari kushirikiana na msanii yeyote katika kutengeneza filamu hizo na kwamba wasingependa kuwalazimisha kufanya hivyo.
“Hatutaki kutoa tangazo la kumwita msanii yeyote, lakini kama kuna mtu anataka kuwa sehemu ya filamu hizo, anakaribishwa,”alisema Aki. “Hatuwezi kuruhusu lugha ya Igbo itoweke.”
Kwa upande wake, Ukwa ambaye pia hujulikana kwa jina la Pawpaw alisema, magazeti mengi yameripoti kwamba yeye na Aki hawapo karibu tena wakati si kweli.
“Huu ni uongo. Unaweza kuona nilikuwa mpambe wake wakati wa harusi yake na kwa sasa tunajiandaa kutengeneza filamu kwa lugha ya Igbo kwa sababu tumegundua lugha hiyo inataka kutoweka,”alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment