KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 19, 2012

Zambia vs Senegal ni pambano la kufa mtu kesho

Mamadou Niang-Senegal

Chris Katongo (kushoto) wa Zambia

Sami Aboud-Libya

ROBOFO Bodipo-Equatorial Guinea


LIBREVILLE, Gabon
MICHUANO ya fainali za soka za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mwaka 2012, inatarajiwa kuanza kutimua vumbi keshokutwa kwa mechi mbili zitakazochezwa kwenye viwanja viwili tofauti.
Katika mechi hizo za kundi A, wenyeji Equatorial Guinea watamenyana na Libya wakati vigogo Senegal watavaana na Zambia.
Pambano kati ya Zambia na Senegal ndilo linalovuta hisia za mashabiki wengi wa soka barani Afrika, kufuatia historia ya nchi hizo na ushiriki wake wa mara kwa mara kwenye fainali hizo.
Senegal, ambayo ni maarufu zaidi kwa jina la Teranga Lions, inashika nafasi ya 44 katika takwimu za ubora duniani na inafundishwa na Kocha Amara Traore. Nahodha wa timu hiyo ni Mamadou Niang.
Hii ni mara ya 12 kwa Simba hao wa Teranga kushiriki kwenye fainali hizo na iliwahi kushika nafasi ya pili katika fainali za mwaka 2002.
Tegemeo kubwa la Traore katika kikosi chake litakuwa kwa washambuliaji wake, Mamadou, Demba Ba, Papiss Demba Cisse na Moussa Sow. Senegal inatumia mfumo wa 4-3-3.
Katika safu yake ya ulinzi, Senegal itawategemea zaidi Bouna Coundoul, anayechezea klabu ya New York Red Bulls ya Marekani, Souleymane Diawara wa Marseille na Kader Mangane wa Rennes za Ufaransa.
Senegal haijawahi kutwaa ubingwa wa Afrika, lakini ni miongoni mwa nchi tatu za Afrika zilizofuzu kucheza raundi ya pili ya fainali za Kombe la Dunia. Zingine ni Cameroon na Ghana.
Kwa upande wa Zambia, inashika nafasi ya 79 kwa ubora wa soka duniani, ikiwa inafundishwa na Kocha Herve Renard. Nchi hiyo imefuzu kucheza fainali za Afrika mara 15 na imewahi kushika nafasi ya pili katika fainali za 1974 na 1994.
Zambia, ambayo ni maarufu zaidi kwa jina la Chipolopolo, imepania kutwaa kombe hilo mwaka huu kwa lengo la kuwaenzi wachezaji wake waliokufa katika ajali ya ndege iliyotokea mwaka 1993 nchini Gabon.
Rais wa Chama cha Soka cha Zambia (FAZ), Kalusha Bwalya alikaririwa hivi karibuni akisema kuwa, lengo lao ni kufika hatua za juu zaidi katika fainali hizo na ikiwezekana kutwaa ubingwa.
Herve ndiye aliyeiongoza Zambia kufuzu kucheza robo fainali katika fainali za mwaka 2010, ikiwa ni hatua ya juu zaidi tangu mwaka 1996.
Kocha huyo kutoka Ufaransa atawategemea zaidi nahodha wake, Chris Katongo na mdogo wake, Felix pamoja na Joseph Musonda, kipa Kennedy Mweene na kiungo Isaac Chansa.
Pambano kati ya Equatorial Guinea na Libya halitarajiwi kuwa na msisimko mkali kwa vile timu zote zinaundwa na wachezaji wasiokuwa na majina. Equatorial Guinea inashika nafasi ya 150 kwa ubora duniani wakati Libya ni ya 63.
Equatorial Guinea, ambayo ni maarufu zaidi kwa jina na Nzalang Nacional ni nchi pekee iliyopewa nafasi ya kuandaa fainali hizo huku ikiwa inashika nafasi za chini zaidi kwa ubora wa soka duniani.
Vijana hao wa Nzalang wananolewa na Kocha Paulo Gilson kutoka Brazil, aliyekabidhiwa kibarua hicho mwanzoni mwa mwezi huu baada ya kutimuliwa kwa kocha wa zamani, Henri Michel.
Mbrazil huyo ameteua wachezaji wengi zaidi wazalendo kwenye kikosi chake huku akiongeza nyota watano wanaocheza nje ya nchi hiyo. Nyota hao ni pamoja na kiungo Juvenal Edjogo-Owono anayecheza soka nchini Hispania.
Nyota wengine wa kulipwa waliomo kwenye kikosi hicho ni Danilo, Doe anayecheza soka Liberia, Narciosse Ekanga anayecheza Cameroon na Ben Konate anayekipiga Ivory Coast. Kikosi cha timu hiyo kitakuwa chini ya nahodha Rodolfo Bodipo, akisaidiana na Javier Balboa.
Kikosi cha Libya, kitashuka dimbani kikiwa chini ya Kocha Marcos Paqueta na nahodha Samir Aboud. Hii ni mara ya tatu kwa Libya kushiriki kwenye fainali hizo na kiliwahi kushika nafasi ya pili katika fainali za mwaka 1982.
Licha ya nchi hiyo kukabiliwa na vita kali ya wenyewe kwa wenyewe, wachezaji wa timu hiyo walicheza kwa ari kubwa na kufanikiwa kufuzu kucheza fainali hizo.
Libya ililazimika kucheza mechi zake mbili za kuwania kufuzu kucheza fainali hizo nje ya nchi hiyo. Mechi hizo zilikuwa dhidi ya Mali na Misri huku ligi ya nchi hiyo ikiwa imesimama tangu Machi mwaka jana. Kocha Paqueta amesema ili kujiweka fiti kwa ajili ya fainali hizo, wachezaji wake wengi walilazimika kwenda kucheza soka ya kulipwa katika nchi za Tunisia na Misri, ambazo nazo pia zilikumbwa na machafuko.
Kwa sasa, Libya ni maarufu zaidi kwa jina la Mediterranean Knights baada ya kuacha kutumia jina la The Greens. Kikosi hicho kitakuwa chini ya nahodha na kipa wake, Samir Aboud, atakayesaidiwa na Ahmed Saad na kiungo Jamal Abdallah.
Katika fainali za mwaka huu, Ghana na Ivory Coast ndizo zinazopewa nafasi kubwa ya kuibuka na ubingwa, kufuatia kukosekana kwa mabingwa watetezi, Misri na vigogo Cameroon, Nigeria, Algeria na Afrika Kusini.
Ghana ilitwaa kombe hilo kwa mara ya mwisho miaka 30 iliyopita wakati Ivory Coast ililitwaa miaka 20 iliyopita. Kila moja imepania kufuta ukame huo kwa kutwaa ubingwa mwaka huu.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya soka wanazipa pia nafasi hizo nchi za Morocco na Burkina Faso, ambazo zilionyesha kiwango cha juu katika mechi za hatua ya awali.

No comments:

Post a Comment