KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 12, 2012

Mogella atoa tahadhari kwa Yanga






00000
MMOJA wa wanasoka waliong’ara nchini miaka ya 1980 hadi 1990 ni Zamoyoni Mogella, ambaye alikuwa maarufu zaidi kwa jina la Golden Ball. Mbali na kuwa mwanasoka nyota enzi hizo, Zamoyoni ni miongoni mwa wachezaji wachache walioweza kunufaika kimaisha kutokana na soka. Katika makala hii ya ana kwa ana iliyoandikwa na ATHANAS KAZIGE, mchezaji huyo anazungumzia masuala mbalimbali kuhusu soka.
00000


SWALI: Wakati ukiwa Simba na baadaye Yanga, mliwahi kupambana na timu mbalimbali kutoka Misri katika michuano ya klabu za Afrika. Nini maoni yako kuhusu mechi ijayo ya klabu bingwa Afrika kati ya Yanga na Zamalek?
JIBU: Ninachoweza kuwashauri viongozi na wachezaji wa Yanga ni kwamba, wajiandae vizuri kabla ya kukabiliana na Zamalek kwa sababu ni timu nzuri na tishio kisoka barani Afrika, ikiwa imewahi kutwaa ubingwa mara kadhaa.
Ni kweli nina uzoefu mkubwa na timu za Misri. Ni timu zenye uzoefu mkubwa na mbinu za kila aina, ndani na nje ya uwanja.
Pia ni timu zenye uwezo mkubwa kifedha na viongozi wao hutoa ahadi nono ya pesa kwa wachezaji wao kila zinapokabiliwa na mechi ngumu na muhimu hiyo ni miongoni mwa sababu zinazozifanya timu zao zifanye vizuri.
Mashabiki wa timu hizo pia wana umoja, hasa timu mojawapo inapokuwa ikiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa, tofauti na hapa kwetu, ambapo mashabiki wa timu moja huweza kuwazomea wapinzani wao na kuwapa nguvu wageni. Kwa Wamisri, hilo halipo kabisa.
Kuna mbinu moja inayotumiwa sana na wachezaji wa Misri ya kujiangusha hovyo uwanjani na iwapo mwamuzi hatakuwa makini, ni rahisi kwa timu yao kushinda, hasa wanapocheza nyumbani.
SWALI: Unadhani ni kipi kinachotakiwa kufanywa na Yanga ili iweze kuitoa Zamalek na kusonga mbele?
JIBU: Mazoezi ndiyo siri pekee ya ushindi. Wachezaji wanapaswa kujifua kwa nguvu zote ili kuhakikisha timu inakuwa fiti. Litakuwa jambo zuri zaidi iwapo timu itapatiwa mechi za kirafiki za kimataifa kabla ya kukabiliana na Zamalek.
SWALI: Kumekuwepo na mgogoro wa chini kwa chini kati ya uongozi, kocha na wachezaji kuhusu mishahara kucheleweshwa. Unadhani hili linaweza kuiathiri Yanga katika mechi hii?
JIBU: Nadhani kuna umuhimu mkubwa kwa wachezaji wa Yanga kuandaliwa kisaikolojia, si kwa sababu ya mgogoro huo, bali pia kuwaandaa wachezaji kimashindano.
Kwa maoni yangu, nadhani wakati umefika kwa Shirikisho la Soka Nchini (TFF) kuajiri mtaalamu wa masuala ya kisaikolojia kwa lengo la kuwaandaa wachezaji wa timu ya taifa na za klabu zinaposhiriki michuano ya kimataifa.
Mtaalamu huyo ni muhimu kwa vile wachezaji wengi wa Tanzania hawajitambui kwamba wana vipaji, ndio sababu wanashindwa kucheza soka kwa miaka mingi. Wengi hustaafu kucheza soka baada ya muda mfupi.
Binafsi ningependa kuona klabu za ligi kuu nazo zinaajiri wataalamu wa aina hii ili ziweze kuwaandaa wachezaji wake kimashindano badala ya ilivyo sasa, ambapo wanashindwa kujitambua na kutambua umuhimu wa soka kwao. Wachezaji wanapaswa kuandaliwa vyema kabla ya mashindano.
SWALI: Kwanini unasisitiza sana suala la wachezaji kuandaliwa kisaikolojia?
JIBU: Nimefanya uchunguzi na kubaini kwamba, timu za Tanzania zinaundwa na wachezaji wengi wazuri na wenye uwezo wa kufika mbali, lakini hawajitambui.
Wapo baadhi ya wachezaji wetu wenye vipaji vya soka kama ilivyo kwa Samuel Eto’o wa Cameroon, lakini wanashindwa kuonyesha uwezo wake kutokana na kutojitambua.
Matokeo yake ni kwamba, vipaji vya wachezaji wetu wengi hufifia baada ya muda mfupi na wengine kuupa kisogo mchezo huo kwa kuona hauna manufaa kwao.
Ninaamini wakiwepo wataalamu wa saikolojia, wataweza kuwasaidia wachezaji na kuwafanya wajitambue na hivyo kuuona mchezo wa soka ni ajira kubwa kwao.
SWALI: Umeshatazama mechi nyingi za michuano ya ligi na zile zinazoihusisha timu ya taifa, Taifa Stars. Umegundua tofauti ipi ya uchezaji enzi zenu na hivi sasa?
JIBU: Tofauti ipo kubwa. Enzi zetu tulikuwa tunacheza soka kwa mapenzi, lakini hivi sasa soka ni pesa. Wachezaji wanalipwa vizuri na kupata zawadi nyingi, hasa wale wa Taifa Stars, lakini inashangaza kuona kuwa, hakuna mafanikio.
Kwa kawaida, mchezaji anatakiwa kulipwa vizuri ili aweze kutimiza malengo yake. Enzi zetu mapenzi ndiyo yaliyotufanya tucheze kwa bidii na kujituma. Wachezaji walikuwa wanajitolea zaidi.
Lakini hivi sasa huwezi kusikia mchezaji anasajiliwa bila kulipwa pesa. Ujio wa baadhi ya wafadhili umesaidia sana kuongeza ushindani, hivyo kinachotakiwa ni kwa wachezaji kuongeza ushindani, kuwa na ari na kujituma.
Enzi zetu timu zilikuwa chache na zilimilikiwa na taasisi mbalimbali za serikali na ndio sababu wachezaji wake walicheza kwa kujituma. Timu kama RTC Kagera, Pamba ya Mwanza, Pilsner na Reli ya Morogoro ni miongoni mwa timu zilizokuwa zikitamba enzi hizo.
Wachezaji wa sasa hawachezi kwa kujituma sana. Wanafanya hivyo pale tu wanapoahidiwa kupewa zawadi. Pia kumezuka matabaka kwenye baadhi ya timu. Kuna wachezaji wanaolipwa pesa nyingi na wanaolipwa pesa kiduchu. Hali hii inachangia kutokuwepo kwa umoja na kushuka kwa ari ya wachezaji.
Kibaya zaidi, wamezuka baadhi ya viongozi, ambao wanaingia madarakani si kwa lengo la kuendeleza soka, bali kujinufaisha wao binafsi. Watu wa aina hii ni hatari kwa maendeleo ya soka.
SWALI: Unapenda kutoa ushauri gani kwa TFF ili yawepo mabadiliko katika uendeshaji soka nchini?
JIBU: Nawashauri viongozi wa TFF wawe makini kuwekeza nguvu zaidi katika kukuza vipaji vya vijana na kuwaendeleza.Hakuna njia ya mkato ya kupata maendeleo zaidi ya kuwekeza katika soka ya vijana.
Nchi nyingi zilizoendelea kisoka barani Afrika, zimepata mafanikio kutokana na kuwekeza kwa vijana. Tazama nchi kama Senegal, Ivory Coast, Ghana na Cameroon, zinatisha kisoka kwa sababu ya kutilia mkazo soka ya vijana. Nasi tunapaswa kuiga mfano huo.
SWALI: Unatoa mwito gani kuhusu watu wanaoingia katika michezo kwa lengo la kujinufaisha?
JIBU: Nawashauri wanachama wa klabu za soka nchini na wajumbe wa vyama vya soka vya wilaya, mikoa na TFF taifa, kuhakikisha wanawachagua watu wenye uwezo, mwelekeo na mapenzi ya soka. Wasithubutu kuwachagua watu wasiokuwa na historia yoyote ya soka, ambao mara nyingi lengo lao ni kujinufaisha wao binafsi badala ya kuleta maendeleo.
Vilevile navishauri vyombo vinavyochuja wagombea katika chaguzi mbalimbali, kutowaonea aibu wagombea wasiokuwa na mwelekeo wa kimichezo. Wanapowaruhusu wagombea wa aina hii kuwania uongozi, ndipo wanapokaribisha matatizo.
Kwa sasa, wapo viongozi wengi wa soka, ambao hawana rekodi zozote za maana, ikiwa ni pamoja na kucheza soka au hata kuongoza timu za mitaani, lakini wanazo pesa nyingi na ndizo zinazowawezesha kushinda nafasi wanazogombea.
SWALI: Ungependa kutoa ushauri gani kwa viongozi wa serikali kuhusu michezo?
JIBU: Naishauri Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuhakikisha michezo inaendelezwa zaidi katika ngazi za shule za msingi, sekondari na vyuo, ambako ndiko chimbuko la wanamichezo. Pia ihakikishe walimu wa michezo wanapatiwa mafunzo ya kitaalamu ili waweze kuinua viwango vya michezo mbalimbali katika ngazi hizo.
Naiomba pia serikali kwakushirikiana na halmashauri za wilaya kuhakikisha wavamizi wote wa viwanja vya michezo wanaondolewa ili kutoa nafasi kwa watoto wetu kuvitumia viwanja hivyo kucheza michezo mbalimbali.

No comments:

Post a Comment