BATA, Equatorial Guinea
HAYAWI hayawi, hatimaye yamekuwa. Michuano ya soka ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika inaanza kutimua vumbi leo kwa mechi mbili za ufunguzi za kundi A zitakazochezwa mjini hapa.
Katika mechi ya kwanza, wenyeji Equatorial Guinea watafungua dimba kwa kumenyana na Libya kabla ya vigogo vya soka barani Afrika, Senegal kuchuana na Zambia.
Mechi zote mbili zinatarajiwa kuwa na ushindani mkali kutokana na maandalizi yaliyofanywa na kila timu, huku zingine zikiwa zimeahidiwa mamilioni ya pesa iwapo zitashinda.
Serikali ya Equatorial Guinea juzi iliahidi kuwazawadia wachezaji wa timu hiyo bonasi ya dola milioni moja za Marekani iwapo wataishinda Libya.
Ahadi hiyo ya pesa imetolewa na mtoto wa rais wa nchi hiyo, Teodoro Obiang Nguema kupitia kwa msemaji wa shirikisho la soka la nchi hiyo.
Msemaji huyo, David Monsuy alisema juzi kuwa, ahadi hiyo imeongeza ari kubwa kwa wachezaji wa timu hiyo kufanya vizuri katika patashika hiyo.
Mbali na kiasi hicho cha fedha, timu hiyo pia imeahidiwa kupewa dola 20,000 za Marekani kwa kila bao itakalofunga katika michuano hiyo.
Equatorial Guinea, maarufu kwa jina la Nzalang Nacional, inanolewa na Kocha Paulo Gilson kutoka Brazil, aliyekabidhiwa kibarua hicho mwanzoni mwa mwezi huu baada ya kutimuliwa kwa kocha wa zamani, Henri Michel.
Mbrazil huyo ameteua wachezaji wengi zaidi wazalendo kwenye kikosi chake huku akiongeza nyota watano wanaocheza nje ya nchi hiyo. Nyota hao ni pamoja na kiungo Juvenal Edjogo-Owono anayecheza soka nchini Hispania.
Kikosi cha Libya, kitashuka dimbani kikiwa chini ya Kocha Marcos Paqueta na nahodha Samir Aboud. Hii ni mara ya tatu kwa Libya kushiriki kwenye fainali hizo na kiliwahi kushika nafasi ya pili katika fainali za mwaka 1982.
Pambano kati ya Zambia na Senegal ndilo linalovuta hisia za mashabiki wengi wa soka barani Afrika, kufuatia historia ya nchi hizo na ushiriki wake wa mara kwa mara kwenye fainali hizo.
Senegal, ambayo ni maarufu zaidi kwa jina la Simba wa Teranga, inashika nafasi ya 44 katika takwimu za ubora duniani na inafundishwa na Kocha Amara Traore. Nahodha wa timu hiyo ni Mamadou Niang.
Tegemeo kubwa la Traore katika kikosi chake litakuwa kwa washambuliaji wake, Mamadou, Demba Ba, Papiss Demba Cisse na Moussa Sow. Senegal inatumia mfumo wa 4-3-3.
Kwa upande wa Zambia, inashika nafasi ya 79 kwa ubora wa soka duniani, ikiwa inafundishwa na Kocha Herve Renard. Nchi hiyo imefuzu kucheza fainali za Afrika mara 15 na imewahi kushika nafasi ya pili katika fainali za 1974 na 1994.
Zambia, ambayo ni maarufu zaidi kwa jina la Chipolopolo, imepania kutwaa kombe hilo mwaka huu kwa lengo la kuwaenzi wachezaji wake waliokufa katika ajali ya ndege iliyotokea mwaka 1993 nchini Gabon.
Kocha huyo kutoka Ufaransa atawategemea zaidi nahodha wake, Chris Katongo na mdogo wake, Felix pamoja na Joseph Musonda, kipa Kennedy Mweene na kiungo Isaac Chansa.
No comments:
Post a Comment