KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, January 25, 2012

PAPIC MAJI SHINGONI, ALIA ATAKUFA NA MTU



KOCHA Mkuu wa Yanga, Kostadin Papic amewekwa kiti moto na uongozi wa klabu hiyo, kufuatia kuwepo na madai ya kuwabagua baadhi ya wachezaji.
Papic aliwekwa kiti moto jana kwenye hoteli ya Serena mjini Dar es Salaam, katika kikao kilichoongozwa na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Lloyd Nchunga, ambapo alitakiwa aeleze iwapo ni kweli anabagua wachezaji.
Mbali na kudaiwa kubagua wachezaji, Papic pia alitakiwa aeleze sababu za Yanga kuvurunda katika mechi yake ya ligi kuu dhidi ya Moro United mwishoni mwa wiki iliyopita.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga na Moro United zilishindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya mabao 2-2.
“Ni kweli tumepanga kumuhoji Papic kuhusu mambo mbalimbali, lakini kubwa tunataka atueleze kwa nini hataki kuwatumia baadhi ya wachezaji,” alisema jana mmoja wa viongozi wa Yanga, alipozungumza na Burudani.
Kiongozi huyo alisema wachezaji, ambao inadaiwa kuwa Papic hataki kuwachezesha ni wale waliosajiliwa na kocha wa zamani wa timu hiyo, Sam Timbe kutoka Uganda.
Kocha huyo mwishoni mwa wiki iliyopita alinsurika kupigwa na baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo, waliokuwa wamelizunguka basi dogo la Yanga lenye namba za usajili T 838 AZM.
Mashabiki hao waliamua kulizunguka basi hiyo baada ya kukerwa na matokeo ya mechi kati ya Yanga na Moro United, ambapo timu hiyo kongwe ilicheza chini ya kiwango.
Baadhi ya mashabiki hao walisikika wakimshutumu kocha huyo kwa kushindwa kupanga timu nzuri na kutowatumia baadhi ya wachezaji, ambao uwezo wao upo juu.
Tayari kocha huyo ameshapewa mechi tatu za kupima uwezo wake na iwapo Yanga itavurunda, huenda akatimuliwa na nafasi yake kuchukuliwa na kocha mwingine.
Uchunguzi zaidi uliofanywa na Burudani umebaini kuwa, wachezaji wa Yanga kwa sasa wamegawanyika katika makundi mawili na hivyo kusababisha hali ya kutokuelewana.
Wakati huo huo, Papic amesema hatamvumilia mchezaji yeyote, ambaye atashindwa kuwajibika ipasavyo na kumsababishia matatizo katika kibarua chake.
Papic alisema hayo jana mara baada ya kumalizika kwa mazoezi ya timu yake yaliyofanyika katika uwanja wa shule ya sekondari ya Loyola iliyopo Mabibo, Dar es Salaam.
Akionekana kutokuwa na masihara, kocha huyo kutoka Serbia alisema, atahakikisha kila mchezaji anawajibika na iwapo atashindwa kufanya hivyo, atafute timu nyingine ya kuchezea.
Papic alisema amekuwa akipokea lawama nyingi kutokana na uzembe wa wachezaji wachache na hivyo kupata matatizo makubwa kwa uongozi, wanachama na mashabiki.
Alisema kuanzia sasa, atahakikisha kila mchezaji anakuwa na nidhamu ya hali ya juu na kutimiza wajibu wake ipasavyo.
"Tumevumiliana vya kutosha, hakuna sababu ya kuendelea kumvumilia mtu ambaye hatimizi wajibu wake ipasavyo, badala yake anakalia maneno tu," alisema Papic.

No comments:

Post a Comment