KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 26, 2012

GYAN: Tulikuwa na bahati kuifunga Botswana


LIBREVILLE, Gabon
MSHAMBULIAJI nyota wa timu ya taifa ya Ghana, Asamoah Gyan amekiri kuwa, ushindi walioupata dhidi ya Botswana ulitokana na bahati.
Ghana iliishinda Botswana idadi hiyo ya bao Jumanne iliyopita katika mechi ya kundi D ya michuano ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika iliyochezwa mjini hapa.
Asamoah alikiri kuwa, yeye na wachezaji wenzake hawakufurahishwa na ushindi huo.
Katika mechi hiyo, Ghana ilikuwa na wakati mgumu kufuatia kupata upinzani mkali kutoka kwa Botswana, ambayo inashika nafasi za chini kwa ubora wa viwango vya soka duniani.
Hata hivyo, Gyan alisema Ghana itaendelea kuimarika kadri michuano hiyo itakavyokuwa ikisonga mbele.
“Tulikuwa na bahati kubwa kushinda, lakini hii inaonyesha hali halisi ya vijana,”alisema.
“Siku zote kila mechi ya kwanza huwa ni ngumu, lakini cha muhimu ni pointi tatu,”aliongeza.
“Nilieleza kabla ya kuanza kwa michuano hii kwamba, tutarajie maajabu mengi kwa sababu timu yoyote inaweza kushinda wakati wowote,”alisema Gyan.
Mchezaji huyo, anayechezea klabu ya Al Ain ya Abu Dhabi, ameahidi kuwa, kikosi chake kitakuwa imara na chenye makali zaidi katika mechi yao ijayo dhidi ya Mali. Mechi hiyo itapigwa kesho.
Mabingwa hao wa zamani mara nne wa Afrika wamepania kufuta ukame wa kushindwa kutwaa kombe hilo katika kipindi cha miaka 30 iliyopita. Kwa mara ya mwisho, walitwaa kombe hilo mwaka 1982.
Gyan alisema ana hakika Mali watacheza mchezo tofauti na wa Botswana, ambayo iliwapa wakati mgumu wa kuipenya ngome yake.
“Kikosi chetu kina uzoefu mkubwa na tunaelewa tunahitaji nini, tumedhamiria kuwapa furaha mashabiki wetu,”alisema.
Katika mechi yao ijayo, Ghana itacheza bila ya beki wake, John Mensah, ambaye anatumikia adhabu ya kukosa mechi moja baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu.

No comments:

Post a Comment