'
Friday, January 27, 2012
Kocha wa Senegal hatarini kutimuliwa
MALABA, Equatorial Guinea
SHIRIKISHO la Soka la Senegal (SFF) limesema, hatma ya Kocha Amara Traore itajulikana baada ya kumalizika kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.
Senegal ni miongoni mwa nchi zilizokuwa zikipewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa, lakini imekuwa ya kwanza kufungasha virago mapema baada ya kupoteza mechi zote mbili za mwanzo.
Katika mechi yake ya kwanza, Senegal ilichapwa mabao 2-1 na wenyeji Equatorial Guinea kabla ya kufungwa idadi hiyo ya mabao na Zambia.
Rais wa SFF, Augustin Senghor alisema juzi kuwa, ni mapema kujadili hatma ya kocha huyo kwa sasa.
“Anapaswa kupewa muda kumaliza michuano. Bado ana mkataba hivyo si jambo zuri kwa sasa kujadili iwapo ataendelea na kibarua chake ama atimuliwe,”alisema.
“Yeye ni kocha katika fainali hizi za Mataifa ya Afrika na baada ya michuano kumalizika, bado mkataba wake utakuwa unaendelea, ambao bado unamweka kwenye kibarua chake. Kila kitu kitaamuliwa baada ya kufanyika tathmini,”aliongeza.
Senghor alisema Traore alipewa malengo kwa ajili ya michuano hiyo, lakini huu si wakati mwafaka kutoa maelezo ya kumkandamiza.
Alisema kocha huyo atalazimika kuwasilisha ripoti yake baada ya michuano hiyo, ambayo itajadiliwa na kamati ya utendaji ya shirikisho hilo na ndiyo itakayoamua hatma yake.
Traore alitia saini mkataba wa kuifundisha Senegal kwa miaka mitatu mwezi uliopita baada ya kufanya mazungumzo na SFF.
Kocha huyo alisema angependa kuendelea na kibarua chake baada ya michuano hiyo, lakini uamuzi wa mwisho upo mikononi mwa shirikisho hilo.
“Hiki ni kikosi cha vijana nab ado kinajengwa na kinahitaji muda zaidi kuimarika,”alisema.
“Sina sababu za kuwalaumu wachezaji wangu, ambao walicheza vizuri na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga mabao,”aliongeza.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment