KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 26, 2012

HAWA NDIO MATAJIRI WA KIKE NOLLYWOOD

Ini Edo

Uche Jombo

Rita Dominick

Genevieve Nnaji

Monalisa Chinda

Funke Akindele

Kate Henshaw

Omotola Jalade

Stephanie Okereke

Mercy Johnson


LAGOS, Nigeria
WAKATI fani ya uigizaji filamu ilipoanza kubisha hodi nchini Nigeria, watu wengi hawakuipa uzito. Ilionekana kama vile ni kazi ya kujifurahisha na isiyo na kipato chochote cha maana.
Lakini miaka michache baadaye, fani hiyo iliyoonekana kuwa ni kichekesho, sasa imeweza kubadili maisha ya watu wengi nchini Nigeria na kuifanya nchi hiyo iwe maarufu barani Afrika na duniani.
Fani hiyo, ambayo ni maarufu zaidi kwa jina la Nollywood, imezifanya filamu za Kinigeria ziwe gumzo duniani kutokana na kubeba uhalisia na upekee wa aina yake. Imetoa ajira kwa raia na wasio raia katika nchi hiyo na kuwafanya baadhi yao wawe matajiri wa kutupwa.
Nollywood imedhihirisha kuwa, Nigeria na bara zima la Afrika hazipaswi kuwekwa pembeni katika masuala ya filamu. Ni fani iliyotoa utambulisho kwa taifa la Nigeria.
Kutokana na umaarufu wa filamu za Kinigeria, baadhi ya waigizaji wake, hasa wa kike, wameweza kujipatia sifa na umaarufu mkubwa, ikiwa ni pamoja na kupewa nafasi ya kucheza filamu za Hollywood.
Lakini kikubwa zaidi ni kwamba, baadhi ya waigizaji hao wa kike hivi sasa ni matajiri na wana mvuto na ushawishi mkubwa kwa jamii. Maisha yao ni ya kifahari, wanamiliki majumba makubwa na kuendesha magari ya starehe.
Ifuatayo ni orodha ya wanawake 18 wa Nollywood, ambao ni matajiri kutokana na kulipwa fedha nyingi kwa kucheza filamu kwa sasa. Lakini utajiri wake hauwezi kuwafikia wacheza filamu wa Hollywood ama Bollywood.
1-INI OBONG EDO- Naira milioni 130
Ini Edo ndiye anayeongoza kwa utajiri miongoni mwa waigizaji nyota nchini Nigeria. Licha ya kukumbwa na vikwazo vingi, mafanikio aliyoyapata hadi sasa ni makubwa, ikiwa ni pamoja na kutayarisha filamu zake mwenyewe. Ni mwigizaji pekee wa kike anayecheza filamu nyingi zaidi kwa mwaka. Kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, picha zake zimekuwa zikitumika kwenye matangazo ya Globacom, Noble Hair na kumwingizia Naira milioni 90. Anamiliki vitega uchumi vingi pamoja na maduka ya nguo na mitindo.
2- UCHE JOMBO- Naira milioni 127
Ni mwigizaji mwenye vituko vingi. Mbali ya uigizaji, pia ni mtayarishaji wa filamu na mfanyabiashara. Rafiki zake wakubwa ni Desmond Elliot, Ini Edo, Monalisa Chinda na Emen Isong. Kwa mwaka 2010, Uche alitengeneza Naira zipatazo milioni 50 kutokana na mikataba mbalimbali na pia kucheza filamu nyingine. Vitega uchumi vyake vingine ni kampuni ya kutengeneza filamu, kampuni ya kuuza na kuagiza bidhaa nje. Ni mwigizaji wa kwanza wa kike kutengeneza filamu yake, ambayo ilimpatia malipo makubwa na kuwafanya wenzake wafuate nyayo zake.
3- RITA DOMINIQUE- Naira milioni 100
Ni mwigizaji wa kike mwenye mvuto zaidi Nollywood, ambaye amekuwa akiingia mikataba ya matangazo na kampuni mbalimbali kama vile Nokia, Globacom na Arik Air.Kwa sasa, anaandaa filamu yake, ambayo inatarajiwa kuanza kuonyeshwa hivi karibuni nchini Nigeria.

4- GENEVIEVE NNAJI- Naira milioni 96
Katika muongo mmoja uliopita, Genevieve ndiye aliyekuwa akiongoza kwa utajiri miongoni mwa waigizaji nyota wa kike nchini Nigeria. Ni mwigizaji mwenye mvuto na anayeheshimika miongoni mwa Wanigeria. Anamiliki kampuni ya mitindo ya mavazi. Na hivi karibuni, Genevieve alikuwa miongoni mwa wacheza filamu waliopewa tuzo ya heshima na Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria. Ndiye msanii anayelipwa fedha nyingi kuliko wote kwa kucheza filamu moja.
5- MONALISA CHINDA- Naira milioni 92
Ni mwigizaji anayetumika kutangaza bidhaa nyingi. Alianza kuitangaza Globacom, ikaja Carnirive na sasa Vita500, kinywaji kinachotengenezwa Korea Kusini.Kama ilivyo kwa Genevieve na Rita, umaarufu wa Monalisa umekuwa ukiongezeka kadri miaka inavyosonga mbele. Na hivi sasa anatengeneza filamu yake, inayojulikana kwa jina la ‘Kiss and Tell’.

6- FUNKE AKINDELE- Naira milioni 90
Inawezekana kwa sasa Funke yupo kwenye kiwango cha juu zaidi. Mwigizaji huyo mwenye kipaji amepata mafanikio kutokana na filamu nyingi alizocheza kuwa na mvuto kwa watazamaji. Alianzia filamu za Yoruba na sasa za Kiingereza. Funke pia ni mfanyabiashara. Filamu yake inayotamba hivi sasa ni The Return of Jenifa, ambayo inatarajiwa kuingiza Naira milioni 40 mwaka huu.
7- KATE HENSHAW – Naira milioni 80
Kuachika kwake kwa mumewe hakujamfanya achuje katika fani ya uigizaji wa filamu. Mwaka 2008, Kate alikuwa mmoja wa wacheza filamu walioshika nafasi za juu kwa utajiri nchini Nigeria na ameendelea kuwa hivyo hadi sasa, japokuwa amezidiwa kete na wengine. Mbali na uigizaji, anamiliki vitega uchumi vya aina mbalimbali.
8- OMOTOLA JALADE EKEINDE – Naira milioni 75
Mwanadada huyu mwenye sura na umbo lenye mvuto, aliyeolewa na rubani wa ndege na kuzaa naye watoto wanne, amecheza filamu nyingi. Mbali na kucheza filamu, Omotola pia ni mwanamuziki na amesharekodi albamu zaidi ya mbili. Mapato yake pia yanatokana na picha za matangazo.
9- STEPHENY OKEREKE- Naira milioni 72
Baada ya kupata mafunzo ya uigizaji katika shule moja ya filamu nchini Marekani, Stepheny amedhihirisha kuwa, chochote kile kinachofanywa na wanaume, wanawake nao wanakiweza. Filamu yake ya kwanza aliyoitengeneza, inayokwenda kwa jina la ‘Through The Glass’ imedhihirisha ukweli huo na kumwezesha kupata tuzo kadhaa za kimataifa. Stepheny pia ni mwanamitindo na muongozaji filamu. Pia ni balozi wa kampuni ya Kenekelon Hair ya Japan.
10- MERCY JOHNSON – Naira milioni 70
Ni mwanadada aliyevamia soko la filamu kwa kasi kubwa. Ni mwigizaji wa pili wa kike kwa umaarufu katika Nollywood baada ya Genevieve. Kuvunjika kwa ndoa yake nusura kummalize, lakini aliweza kusimama imara na kupambana na masaibu yote yaliyomkumba. Kwa kipindi cha mwaka 2007-2010, aliweza kutengeneza zaidi ya Naira milioni 40. Anamiliki vitega uchumi vingi katika mji wa Lagos.

11- CHIOMA CHUKWUKA AKPOTHA – Naira milioni 70
Ni mwigizaji pekee, ambaye hajawahi kukumbwa na skendo ya aina yoyote nchini Nigeria na kamwe huwa hakubali kurudi nyuma. Hivi karibuni, Chioma naye aliamua kujitosa katika kundi la watayarishaji wa filamu wa kike na kucheza katika baadhi ya filamu alizoziandaa. Kwa sasa, anamiliki kampuni yake binafsi ya filamu.
12. OBI EDOZIE – Naira milioni 60
Filamu yake ya ’Save Our Soul’ ilimwezesha kutengeneza zaidi ya Naira milioni 35. Kwa sasa, yupo kwenye hatua za mwisho za kutengeneza filamu ya ’Mr and Mr’. Anachukuliwa kama mfanyabiashara mzuri zaidi kuliko mwigizaji filamu.
13- OMONI ONOBOLI – Naira milioni 54
Ameendelea kupanda kwenye chati za juu katika fani ya uigizaji filamu nchini Nigeria na anatarajiwa kufanya mambo makubwa zaidi katika miaka michache ijayo. Mbali na uigizaji, Omoni pia ni mtayarishaji wa filamu na mwandishi mahiri wa muswada wa filamu. Hivi karibuni, Omoni aliteuliwa kuwa balozi wa detol.
14- OGE OKOYE – Naira milioni 45
Licha ya kutoonekana kwa muda mrefu, Oge ameweza kupata mafanikio makubwa katika uigizaji kutokana na umahiri na umakini wake katika kazi hiyo. Kwa sasa, Oge analipwa pesa nyingi kutokana na uigizaji kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma na amepania kurejea kwenye chati za juu.
15- TONTO DIKE- Naira milioni 27
Umchukie ama umpende, ukweli ni kwamba Tonto ni mmoja wa waigizaji maarufu na wenye mvuto katika Nollywood kwa sasa kama ilivyo kwa Mercy. Skendo zilizowahi kumkumba kimaisha ndizo zilizozidi kumuongezea umaarufu. Mbali ya uigizaji, Tonto anafanya biashara mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuagiza magari nje ya nchi.
16- EMPRESS NJAMAH – Naira milioni 20
Mapato ya Empress hayatokani na uigizaji wa filamu pekee, bali pia kutokana na uanamitindo wa mavazi, upambaji wa maharusi, uagizaji wa bidhaa kutoka nje na umiliki wa ardhi.

17- CHIKA IKE – Naira milioni 15
Anaweza kuonekana si maarufu, lakini amekuwa mmoja wa wachezaji filamu wenye mafanikio makubwa kwa sasa katika Nollywood. Pia anamiliki duka kubwa la mavazi katika mji wa Abuja, linalokadiriwa kuwa na thamani ya Naira milioni saba.

18- HALIMA ABUBAKAR – Naira milioni 10
Ni mwigizaji mwenye sura na umbo lenye mvuto, akiwa anafanya vizuri kwenye fani. Anamiliki nyumba kadhaa za kifahari. Kwa sasa anajiandaa kutengeneza filamu yake mwenyewe, inayotarajiwa kuanza kuonyeshwa hivi karibuni.

1 comment:

  1. great.i like em all nigerian diva celebrity.keep goin ladies.

    ReplyDelete