KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 19, 2012

RC Arusha awashukia viongozi wa ARFA, JKT Oljoro yachangiwa mil 15/-


Na Shaaban Mdoe, Arusha
MKUU wa mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo ametangaza vita dhidi ya viongozi wa Chama cha Soka mkoa wa Arusha (ARFA) kwa kushindwa kusimamia mchezo mkoani hapa na pia kuitelekeza timu JKT Oljoro inayoshiriki michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Mulongo amesema atafanya kila analowezesha kuhakikisha viongozi wa ARFA waliopo madarakani hivi sasa hawarudi tena katika uchaguzi ujao kwa vile wameshindwa kutekeleza majukumu yao.
Mkuu huyo wa mkoa alitoa kauli huyo jana mjini hapa alipokuwa akizungumza na wachezaji wa JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini hapa kwa ajili ya kuwatakia heri katika mechi za mzunguko wa pili wa ligi zinazotarajiwa kuanza keshokutwa.
Alisema kwa muda wa miezi mitano sasa tangu ateuliwe kuwa mkuu wa mkoa wa Arusha, hajawahi kuona kiongozi hata mmoja wa chama hicho akijitambulisha kwake ama kuitambulisha JKT Oljoro kwa ajili ya kuipangia mikakati.
Mulongo alisema kutokana na kasoro hiyo, inaonyesha wazi kuwa, viongozi hao hawaiungi mkono timu hiyo pekee ya mkoa wa Arusha inayoshiriki katika ligi kuu na hivyo wachezaji na viongozi wake kuwa hatarini kupoteza ari.
Aliwataka viongozi wa chama hicho kumuandalia mikakati ya kuinua soka mkoani humo na kuiwasilisha kwake kwa ajili ya kuijadili na kuitekeleza kwa vitendo.
"Kazi yenu ni kuvaa beji tu vifuani na kuingia uwanjani bure kutazama mechi za soka. Hatukuwachagua mfanyekazi hizo, tunataka uwajibikaji,"alisema.
Mkuu wa mkoa alisema, alisema kama kuna kiongozi ameshindwa kutimiza wajibu wake ni vyema akaachia nafasi anayoshikilia ili aingie kiongozi mwingine mwenye nia thabiti ya kuongoza soka mkoani Arusha, la si hivyo atafanya kampeni kuhakikisha wanaondoka wote.
Amewataka wachezaji wa JKT Oljoro kujituma na kuacha kubweteka na sifa au mafanikio madogo wanayoyapata ili kutowavunja moyo baadhi ya wadau wachache, ambao wameanza kuonyesha nia ya kuisaidia timu yao .
Wadau hao wameichangia timu hiyo sh. milioni 15 ili kuiwezesha ishiriki vyema katika mechi za mzunguko wa pili wa ligi hiyo. Mkuu wa mkoa na pamoja na rafiki zake walichangia kiasi cha shilingi milioni tano, wilaya sita za mkoa huo zilichangia shilingi milioni nne, mamlaka ya maji safi na maji taka shilingi milioni moja wakati benki ya NMB imetoa pea mbili za jezi na mipira mitano.
Wadau wengine akiwemo mfanyabiashara maarufu wa bidhaa za vyakula toka kampuni ya Alfa Group, Karim Dalia alichangia shilingi milioni mbili huku akiahidi kuongeza sh. milioni 10 zingine iwapo timu hiyo itashika moja ya nafasi tatu za juu wakati mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite ambae pia ni diwani wa kata ya Mbughuni wilayani Arumeru, Mathias Manga amechangia sh. milioni moja..
Wengine ni mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite wa Arusha, Hussein Gonga aaliyechangia shilingi milioni moja, Papa Kinyi, ambae ni mmiliki wa kituo cha redio cha Tripple A, aliyechangia shilingi milioni moja na Meya wa Arusha, Gaudance Lyimo aliyechangia shilingi 500,000.
Mbali na michango hiyo, pia ipo ahadi ya viatu pea 30 kutoka kwa moja ya hoteli kubwa jijini Dar es salaam. JKT Oljoro itaanza mzunguko wa pili wa ligi kwa kumenyana na Mtibwa Sugar keshokutwa.

No comments:

Post a Comment