'
Thursday, January 12, 2012
Wachezaji Botswana wafuta mgomo
GABORONE, Botswana
WACHEZAJI wa timu ya soka ya taifa ya Gabon wameamua kufuta mgomo wao baada ya kuelezwa kuwa, serikali haina pesa za kuwalipa bonasi kwa ajili ya ushiriki wao katika fainali za Afrika.
Rais wa nchi hiyo, Ian Khama amewataka wachezaji wa timu hiyo kuweka utaifa na uzalendo mbele zaidi kuliko maslahi yao binafsi.
Timu hiyo iligoma kufanya mazoezi na kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Zimbabwe kwa madai ya kutolipwa posho mbalimbali.
Wachezaji wa timu hiyo walikuwa wakitaka walipwe zaidi ya dola 13,000 za Marekani kila mmoja kwa ajili ya kushiriki kwenye fainali hizo na malipo mengine kadri watakavyosonga mbele.
Hata hivyo, Chama cha Soka cha Botswana (BFA) kilisimama imara, kikisema kuwa, hakiweza kuwalipa malipo zaidi wachezaji hao.
“Inasikitisha kwamba, katika hatua za mwisho kabla ya safari, wachezaji hawana uhakika kuhusu bonasi zai,” alisema mchezaji nyota wa timu hiyo, Dipsy Selolwane alipohojiwa na BBC juzi.
Mchezaji huyo alisema, kiasi cha pesa walichotaka walipwe ni kidogo na walipokataliwa, walitakiwa kuchagua moja, kubaki ama kurejea nyumbani.
BFA imeahidi kuwalipa wachezaji hao posho zao mwishoni mwa wiki hii baada ya kuchelewa kufanya hivyo wiki iliyopita.
“Hali ilikuwa mbaya, lakini nafurahi kwa sababu tatizo hilo limeshapatiwa ufumbuzi,”alisema Kocha Mkuu wa timu hiyo, Stanley Tshosane.
“Nimezungumza na wachezaji na BFA imezungumza nao na tumekubaliana kwamba, njia pekee sasa ni kusonga mbele,”aliongeza.
Rais Khama mwishoni mwa wiki iliyopita aliwaandalia wachezaji wa timu hiyo chakula cha usiku na bila kutaka kuzungumzia mgomo wao, aliwataka kuweka mbele zaidi utaifa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment