BAADA ya mapumziko ya takriban miezi miwili, timu 14 zinazoshiriki katika michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara zinatarajiwa kurejea tena vitani mwishoni mwa wiki hii.
Katika mechi hizo za mzunguko wa pili zinazotarajiwa kuanza keshokutwa, mabingwa watetezi Yanga watamenyana na Moro United kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Vigogo vingine vya soka nchini, Simba vitauanza mzunguko huo Jumatano ijayo kwa kumenyana na Coastal Union kwenye uwanja huo huo.
Pambano kati ya Yanga na Moro United linatarajiwa kuwa kali na gumu, kufuatia timu hizo kushindwa kutambiana katika mechi ya mzunguko wa kwanza baada ya kutoka sare ya bao 1-1.
Yanga itashuka dimbani huku hali ikiwa si shwari katika klabu hiyo, kufuatia uongozi kuchelewa kuwalipa wachezaji mishahara yao, hali iliyosababisha watishie kugoma.
Hata hivyo, Kocha Mkuu wa Yanga, Kostadin Papic amejigamba kwa kusema kuwa, kikosi chake kipo tayari kwa ligi hiyo na wachezaji wana ari kubwa ya kutetea ubingwa wao.
Kwa upande wa Simba, Kocha Milovan Cirkovic amesema michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyofanyika Zanzibar hivi karibuni ilimwezesha kutambua uwezo wa wachezaji wake na hivyo kukisuka upya kikosi hicho.
Katika mechi ya kwanza kati ya Simba na Coastal Union iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, vijana wa Msimbazi waliibuka na ushindi kiduchu wa bao 1-0.
Katika mechi zingine zitakazochezwa keshokutwa, Mtibwa Sugar itacheza na JKT Oljoro kwenye uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro; Ruvu Shooting itavaana na Toto African kwenye uwanja wa Mlandizi mkoani Pwani wakati Villa Squad itaikaribisha Kagera Sugar kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea Jumapili wakati JKT Ruvu itakapomenyana na Polisi Dodoma kwenye uwanja wa Chamazi wakati Jumatano ijayo, African Lyon itavaana na Azam kwenye uwanja huo huo.
Timu hizo zitauanza mzunguko wa pili huku Simba ikiwa inaongoza ligi kwa kuwa na pointi 28 baada ya kucheza mechi 13, ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 27 na Azam yenye pointi 23.
JKT Oljoro inashika nafasi ya nne kwa kuwa na pointi 23, sawa na Azam, lakini zinatofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.
Chini ya JKT Oljoro ipo timu ya Mtibwa Sugar yenye pointi 22, ikifuatiwa na JKT Ruvu yenye pointi 17, Kagera Sugar yenye pointi 16, Moro United na African Lyon zenye pointi 14 kila moja.
Toto African na Ruvu Shooting zinashika nafasi ya 10 na 11 zikiwa na pointi 13 kila moja, zikifuatiwa na Coastal Union yenye pointi 11 na Polisi Dodoma yenye pointi tisa. Villa Squad inashika mkia kwa kuambulia pointi tisa.
MSIMAMO LIGI KUU YA BARA BAADA YA MZUNGUKO WA KWANZA
P W D L GF GA PTS
Simba SC 13 8 4 1 21 8 28
Yanga 13 8 3 2 20 9 27
Azam 13 6 5 2 12 5 23
JKT Oljoro 13 6 5 2 10 6 23
Mtibwa Sugar 13 6 4 3 17 12 22
JKT Ruvu 13 3 8 2 15 14 17
Kagera Sugar 13 3 7 3 13 12 16
Moro United 13 3 5 5 18 23 14
African Lyon 13 3 5 5 11 16 14
Toto African 13 2 7 4 14 16 13
Ruvu Shooting 13 2 7 4 11 13 13
Coastal Union 13 3 2 8 11 18 11
Polisi Dodoma 13 1 6 6 10 15 9
Villa Squad 13 1 4 8 10 26 7
No comments:
Post a Comment