'
Thursday, January 26, 2012
Nando sasa ruksa kuichezea Angola
MALABO, Equatorial Guinea
MSHAMBULIAJI Nando Rafael wa Angola ameruhusiwa kuichezea timu hiyo katika michuano ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limethibitisha kuwa, Nando aliyeichezea timu ya taifa ya vijana wa chini ya miaka 21 ya Ujerumani, anaruhusiwa kisheria kuichezea Angola.
Nando hakuichezea Angola katika mechi yake ya ufunguzi dhidi ya Burkina Faso, iliyochezwa Jumatatu iliyopita, ambapo timu hiyo ilishinda bao 1-0.
Shirikisho la Soka la Angola (FAF), lilianza kufuatilia taratibu za kumuombea ruhusa hiyo Nando wiki iliyopita.
Kwa uamuzi huo wa FIFA, Nando alitarajiwa kushuka dimbani jana katika mechi ya kundi B dhidi ya Sudan.
“Ninayo furaha kubwa kuwepo hapa na nipo tayari wakati kocha atakaponihitaji, nadhani nitakuwa na msaada mkubwa kwa timu,” alisema Nando juzi alipohojiwa na BBC.
“Jambo la muhimu ni kwamba nipo fiti na nimekuwa nikifanya mazoezi na wenzangu na nimejifunza mambo mengi kwa sababu kila kitu ni kipya kwangu,”aliongeza.
Nando (28) hajawahi kuichezea Angola katika michuano mikubwa, lakini amesisitiza kuwa, siku zote alikuwa na uhakika wa kupata nafasi hiyo.
Kamati ya Haki za Wachezaji ya FIFA ilikutana Jumanne iliyopita mjini Zurich, Uswisi kujadili maombi hayo ya Angola na kuamua kuwa, kwa sasa Nando anaruhusiwa kisheria kuichezea timu hiyo.
Kocha Mkuu wa Angola, Lito Vidigal alisema maandalizi ya timu yake katika mechi ijayo hayatabadili, kufuatia uamuzi wa kumruhusu Nando kuichezea timu hiyo.
“Rafael ni mmoja wa wachezaji 23 kwenye kikosi changu na kama wachezaji wengine, kama anayo nafasi ya kucheza, atacheza,”alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment