KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, January 18, 2012

Bakhresa: Mataji zaidi yanakuja Azam



WACHEZAJI wa Azam wakiwa wamembeba juu kocha wao, Stewart Hall mara baada ya timu hiyo kuichapa Jamhuri ya Pemba mabao 3-1 katika mechi ya fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi, iliyochezwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar. (Picha kwa hisani ya tovuti ya Azam).


MWENYEKITI wa klabu ya Azam, Abubakar Bakhressa amesema ushindi wa timu hiyo katika michuano ya Kombe la Mapinduzi umefungua njia ya kutwaa mataji zaidi.
Abubakar alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa mapokezi ya timu hiyo iliporejea Dar es Salaal ikitokea Zanzibar, ambako ilitwaa kombe hilo.
Azam ilinyakua kombe hilo baada ya kuichapa Jamhuri ya Pemba mabao 3-1 katika mechi kali ya fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Amaan.
Kabla ya kuifunga Jamhuri, Azam iliitoa Simba kwa kuichapa mabao 2-0 katika mechi ya nusu fainali baada ya kuitungua Yanga maba 3-0 katika mechi ya mwisho ya makundi.
Mwenyekiti huyo wa Azam alisema lengo la timu yake ni kutwaa mataji mengi zaidi, ikiwa ni pamoja na ubingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara.
Aliwataka wachezaji wa timu hiyo kuongeza bidii na kucheza kwa kujituma zaidi ili waweze kutimiza lengo lao la kutwaa ubingwa wa ligi kuu.
Azam ilipokewa kwa shangwe kubwa na viongozi wa timu hiyo pamoja na mashabiki waliofurika kwenye gati ndogo ya abiria eneo la bandarini, Dar es Salaam.
Wakati huo huo, Kocha Mkuu wa Azam, Stewart Hall amesema, ubingwa wa michuano ya Kombe la Mapinduzi umewasafishia njia ya kutwaa taji la ligi kuu.
Akizungumza mjini hapa kabla ya kurejea Dar es Salaam, kocha huyo kutoka Uingereza alisema, kwa sasa wameelekeza akili zao kwenye ligi hiyo.
Azam inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 23 baada ya kucheza mechi 13, nyumba ya Simba inayoongoza kwa kuwa na pointi 28 ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 27.
Stewart alisema michuano hiyo ilikuwa mazoezi mazuri kwa timu yake kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa ligi kuu, inayotarajiwa kutimua vumbi kuanzia keshokutwa.
Azam itafungua dimba la mzunguko huo kwa kumenyana na African Lyon katikati ya wiki ijayo kabla ya kuvaana na Moro United katika mechi itakayopigwa Januari 29 mwaka huu. Mechi zote mbili zitachezwa kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment