KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, January 27, 2012

Angola, Sudan zashindwa kutambiana



MSHAMBULIAJI Didier Drogba (kushoto) wa Ivory Coast akianguka baada ya kuliwa kwanja na beki Charles Kabore wa Burkina Faso timu hizo zilipomenyana juzi katika mechi ya michuano ya fainali za Kombe la Afrika.


MALABO, Equatorial Guinea
SUDAN na Angola juzi zilishindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 katika mechi ya kundi B ya michuano ya soka ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika iliyochezwa mjini hapa.
Mshambuliaji Ahmed Bashir aliibuka shujaa wa Sudan baada ya kuifungia mabao yote mawili, yakiwa ni mabao ya kwanza kwa nchi hiyo katika fainali hizo kwa miaka 36 iliyopita.
Angola ndiyo iliyotangulia kufunga bao kupitia kwa mshambuliaji wake nyota, Manucho dakika ya tano baada ya kumpokonya mpira beki Nagmaldien Abdullah wa Sudan.
Bashir aliisawazishia Sudan dakika ya 30 baada ya kuwatoka mabeki wawili wa Angola na kufumua shuti lililotinga moja kwa moja wavuni. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.
Manucho aliiongezea Angola bao la pili kwa njia ya penalti muda mfupi baada ya kuanza kwa kipindi cha pili baada ya Mateus kuangushwa ndani ya eneo la hatari.
Akitumia udhaifu wa mabeki wa Angola, Bashir aliisawazishia Sudan dakika ya 73 kwa shuti kali akiwa ndani ya eneo la hatari la timu pinzani.
Pambano hilo lilihudhuriwa na watazamaji wachache, tofauti na ilivyokuwa katika pambano kati ya Ivory Coast na Burkina Faso, ambapo mashabiki wengi walikuwa na kiu ya kuwaona wachezaji wanaocheza soka ya kulipwa nchini Uingereza.
Sudan, mabingwa wa michuano hiyo mwaka 1979, walifunga bao kwa mara ya mwisho katika fainali za mwaka 1976 zilizofanyika Zaire.
Tangu wakati huo, Sudan imefuzu kucheza fainali hizo mara moja mwaka 2008, ambapo ilifungwa katika mechi zote tatu kwa kipigo cha mabao 3-0 katika kila mechi.
Wachezaji wote 23 waliomo kwenye kikosi cha Sudan, wanacheza soka katika ligi ya nchi hiyo, wakiwemo wachezaji saba wanaochezea klabu ya Al Hilal.

No comments:

Post a Comment