BAADHI ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wamejitokeza kuendesha harambee kwa ajili ya kuichangia timu ya soka ya taifa ya wanawake, Twiga Stars ili iweze kufanya vizuri katika mechi yake ya marudiano ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Afrika dhidi ya Namibia, itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Wabunge hao walisema hayo jana walipokuwa wakihojiwa katika kipindi cha Leo Tena cha kituo cha Clouds FM. Pichani, kutoka kulia ni mbunge wa viti maalum (CCM), ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Watoto, Ummy Ally Mwalimu, wa tatu kulia ni mbunge wa viti maalum CCM, Vicky Kamata, mbunge viti maalum, Zainab Kawawa, mbunge wa viti maalumu CHADEMA, Grace Kihwelu na mbunge wa viti maalumu CCM, Zainabu Vulu. Wa pili kulia ni mtangazaji wa kipindi cha Leo Tena, Dina Marios. (Picha kwa hisani ya blogu ya Michuzi).
WABUNGE wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo wanatarajiwa kuipatia misaada mbalimbali timu ya soka ya taifa ya wanawake, Twiga Stars.
Michango hiyo ya wabunge itatolewa mara baada ya kumalizika kwa mechi ya kirafiki kati ya Twiga Stars na wabunge, itakayochezwa kwenye uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Twiga Stars inajiandaa kwa mechi yake ya marudiano ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Afrika dhidi ya Namibia. Mechi hiyo inatarajiwa kupigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mechi ya awali iliyochezwa wiki iliyopita mjini Whindoek, Twiga Stars iliichapa Namibia mabao 2-0. Ili isonge mbele, inahitaji sare ya aina yoyote katika mechi ya Jumapili.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema jana kuwa, msaada utakaotolewa na wabunge kwa timu hiyo bado haujajulikana.
Alisema Twiga Stars inatarajiwa kurudi Dar es Salaam leo mchana, ikitokea Mlandizi mkoani Pwani, ambako ilikwenda kuweka kambi kwa ajili ya mechi hiyo.
“Mechi ya Twiga Stars na wabunge ni ya kujifurahisha na itachezwa kwa muda mfupi,”alisema Wambura.
Wachezaji waliomo kwenye kikosi cha Twiga Stars ni Sophia Mwasikili , Fatuma Bushiri Fatuma Omari, Mwajuma Abdallah , Asha Rashid, Mwanahamisi Omari, Ettoe Mlenzi, Zena Khamis, Fatuma Khatib, Maimuna Said na Fadhila Hamad.
Wengine ni Fatuma Mustapha, Rukia Hamisi, Mwapewa Mtumwa, Judith Hassan, Aziza Mwadini, Sabai Yusuf, Semeni Abeid, Pulkaria Charaji, Mwanaidi Hamisi, Hanifa Idd na Fatuma Gotagota.
No comments:
Post a Comment