'
Saturday, January 28, 2012
Twiga Stars watishia kugomea mechi yao na Namibia kesho
SIKU moja kabla ya timu ya soka ya taifa ya wanawake, Twiga Stars kushuka dimbani kumenyana na Namibia katika mchezo wa marudiano wa raundi ya kwanza wa kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, wachezaji wa timu hiyo wametishia kugoma.
Wakizungumza mjini Dar es Salaam jana kwa masharti ya kutotajwa majina yao, wachezaji hao walisema, wamefikia uamuzi huo kutokana na kulipwa pesa kidogo za posho kutoka katika sh. milioni saba walizopewa na wabunge.
Wachezaji hao walisema, mara baada ya wabunge kuwakabidhi fedha hizo juzi jioni, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jana asubuhi liliwagawia sh. 100,000 kila mchezaji na kufanya jumla ya malipo kwa wachezaji wote waliopo kambini kuwa sh. milioni tano.
Kwa mujibu wa wachezaji hao, kiasi cha pesa kilichotolewa kwa kila mchezaji, hakiendani na hesabu ya sh. milioni saba zilizotolewa na wabunge. Walisema wanashangaa kuona kuwa, TFF imepiga panga sh. milioni mbili bila kuwapa maelezo yoyote.
"Tulipokabidhiwa zile fedha juzi, wabunge walisema shilingi milioni saba ni kwa ajili ya posho za wachezaji na sh. milioni tatu zitakwenda TFF, sasa TFF wamechukua fedha zao na pia wametukata shilingi milioni mbili zetu, jambo hili limetuuma sana," alisema mmoja wa wachezaji hao.
Wachezaji hao walisema kukatwa kwa pesa hizo kumepunguza morali waliyokuwa nayo kwa ajili ya mechi yao na Namibia na kuongeza kuwa, wamekuwa wakicheza kwa kujituma na kutumia nguvu zaolakini wanaishia kukatishwa tamaa.
Kwa mujibu wa hesabu za wachezaji hao, kikosi chao kina wachezaji 20 hivyo kutokana na sh. milioni saba walizopewa na wabunge, kila mmoja alistahili kupata zaidi ya sh. 100,000 walizopewa na TFF.
Wakati akikabidhi pesa hizo kwa wachezaji, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu aliwaasa viongozi wa TFF wasichakachue fedha hizo kwa vile zimetolewa kwa ajili ya wachezaji tu.
Twiga Stars inatarajiwa kurudiana na Namibia kesho katika mechi itakayopigwa kuanzia saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mechi ya awali, iliyochezwa wiki mbili zilizopita mjini Whindhoek, Twiga Stars ilishinda mabao 2-0. Ili isonge mbele, inahitaji sare ya aina yoyote.
Akizungumzia malalamiko hayo ya wachezaji wa Twiga Stars, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, alisema yamewasikitisha kwa vile wameshindwa kuelewa mchanganuo wa fedha hizo, ambazo walizipokea wenyewe.
Wambura alisema fedha hizo zilipokelewa na nahodha wa timu hiyo, Sophia Mwasikili, ambaye alizikabidhi kwa Meneja wa timu, Furaha Francis, ambaye naye aliziwasilisha kwa Mkurugenzi wa Fedha wa TFF, Ahmed Naheka.
Alisema fedha hizo ziliwasilishwa kwa Naheka ili ziingizwe katika hesabu za TFF na pia zionekane zimetoka kwa ajili gani ili wakaguzi wajue mapato na matumizi ya fedha za shirikisho hilo.
Wambura alisema TFF iliamua kuwapa wachezaji sh. milioni tano kati ya sh. milioni saba, zikiwa ni posho zao kwa siku saba na sh. milioni mbili zilikatwa kwa lengo la kufidia posho zao za siku tano, ambazo tayari shirikisho hilo lilikuwa limeshawalipa.
Ofisa huyo alisema hakuna kilichoharibika kwa wachezaji kulipwa fedha hizo kwa sababu zile zilizotolewa na wabunge zilikuwa za siku 13 na kwamba TFF imekuwa ikigharamiachakula na mahitaji mengine ya timu hiyo, ambayo imekuwa ikikaa bure katika kambi ya Jeshi.
"TFF inatoa fedha kwa ajili ya chakula wanachokula, tumenunua mashuka na vyandarua, hivyo si kwamba wanakaa bure katika kambi hiyo, fedha zinazopatikana pia zinahudumia maeneo mengine," alisema Wambura.
Wakati huo huo, Bodi ya Dawa nchini imetoa sh. milioni 10 kwa ajili ya timu hiyo ukiwa mwendelezo wa kuisaidia wakati Chama cha Mapinduzi wilaya ya Ilala kimetoa katoni 10 za maji zenye thamani ya sh. 26,000.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment