KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, January 27, 2012

Ivory Coast yatinga robo fainali

KIUNGO Yaya Toure (kushoto) wa Ivort Coast akidhibitiwa na beki Mahamadou Kere wa Burkina Faso, timu hizo zilipomenyana juzi katika mechi ya kundi B ya michuano ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika iliyochezwa mjini Malabo. Ivory Coast ilishinda mabao 2-0.



MALABO, Equatorial Guinea
IVORY Coast juzi ilifuzu kucheza robo fainali ya michuano ya soka ya Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kuichapa Burkina Faso mabao 2-0 katika mechi ya kundi B iliyochezwa mjini hapa.
Matokeo hayo yaliiwezesha Ivory Coast kuongoza kundi hilo ikiwa na pointi sita baada ya kucheza mechi mbili, ikifuatiwa na Angola yenye pointi nne na Sudan yenye pointi moja. Burkina Faso bado haijaambulia pointi na imeshatolewa hatua za awali.
Angola na Sudan sasa zinagombea nafasi moja iliyosalia ya kufuzu kucheza robo fainali kutoka kundi hilo, ambapo kila moja italazimika kushinda mechi za mwisho.
Katika mechi hizo zitakazochezwa Jumatatu ijayo, Sudan itamenyana na Burkina Faso mjini Bata wakati Angola itavaana na Ivory Coast mjini Malabo.
Mshambuliaji Salomon Kalou aliifungia Ivory Coast bao la kuongoza dakika ya 16 baada ya kupokea krosi kutoka kwa Yaya Toure na kufumua shuti lililompita kipa Daouda Diakite.
Bao la pili la Ivory Coast lilitokana na uzembe wa beki Bakary Kone wa Burkina Faso kujifunga dakika ya 82 wakati akiwa kwenye harakati za kuokoa hatari iliyoelekezwa kwenye lango la timu yake.
Katika mechi hiyo, Ivory Coast ilimchezesha kwa mara ya kwanza mshambuliaji wake, Didier Zokora baada ya kukosa mechi ya awali dhidi ya Sudan kutokana na kutumikia adhabu ya kufungiwa. Zokora alichukua nafasi ya Igor Lolo.
Licha ya safu ya ushambuliaji ya Ivory Coast kuundwa na washambuliaji wake nyota kama vile, Didier Drogba, Kalou na Gervinho, ilipata wakati mgumu wa kuipita ngome ya Burkina Faso na hivyo kumpa kazi kubwa kiungo wake Yaya Toure kuhaha huku na huko.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Kocha Mkuu wa Burkina Faso, Paulo Duarte alieleza kusikitishwa kwake kutokana na kupoteza mechi hiyo.
Hata hivyo, Duarte alikataa kuzungumzia hatma yake kwa madai kuwa, walifungwa kwa bahati mbaya na si kwa kuzidiwa kimchezo.
Kocha Mkuu wa Ivory Coast, Francois Zahoui alisema ameridhishwa na ari waliyonayo vijana wake, lakini alikiri kuwa, bado wanahitajika kuwa makini zaidi katika mechi zijazo.

No comments:

Post a Comment