'
Thursday, January 26, 2012
Mtoto wa rais Eq Guinea awamwagia mapesa wachezaji
BATA, Equatorial Guinea
MTOTO wa Rais wa Equatorial Guinea, Teodoro Nguema Obiang Mangue ametimiza ahadi aliyotoa kwa wachezaji wa timu ya taifa ya nchi hiyo baada ya kuwakabidhi zawadi ya dola milioni moja za Marekani (sh. bilioni 150).
Teodoro alitoa ahadi hiyo kabla ya kuanza kwa michuano ya fainali za Kombe la Afrika, ambapo aliahidi kuizawadia timu hiyo kiasi hicho cha fedha wakishinda mechi yao ya ufunguzi dhidi ya Libya.
Mbali na ahadi hiyo, Teodoro pia aliahidi kuizawadia timu hiyo dola 20,000 za Marekani (sh. milioni 30) kwa kila bao watakalofunga.
Katika mechi ya ufunguzi iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita, Equatorial Guinea iliichapa Libya bao 1-0 na juzi iliifunga Senegal mabao 2-1.
Mtoto huyo wa rais aliwakabidhi wachezaji wa Equatorial Guinea kitita hicho katika hafla iliyofanyika Jumanne iliyopita. Teodoro alikabidhi hundi ya kiasi hicho cha pesa kwa nahodha wa timu hiyo, Juvenal Edjogo.
Mshambuliaji Javier Balboa, aliyeifungia timu hiyo bao pekee na la ushindi katika mechi dhidi ya Libya, naye alikabidhiwa dola 20,000.
Mwingine aliyezawadiwa dola 20,000 ni Ivan Bolado, ambaye alifunga bao kipindi cha kwanza katika mechi dhidi ya Libya, lakini likakatiwa na mwamuzi kwa vile alikuwa ameotea.
Mtoto huyo wa rais ameahidi kuwazawadia pesa nyingine wachezaji wa timu hiyo iwapo watashinda mechi zijazo za kundi A.
Hii inamaanisha kwamba, wachezaji wa Equatorial Guinea watazawadiwa dola zingine milioni moja kwa kuishinda Senegal na dola 40,000 kwa mabao yaliyopatikana katika mechi hiyo.
Zawadi aliyotoa mtoto huyo wa rais kwa kikosi cha Equatorial Guinea, imezua utata kwa baadhi ya wanaharakati, ambao wameupongeza uamuzi wake huo, lakini wanahoji amepata wapi pesa hizo.
Mwaka jana, serikali ya Marekani ilianzisha uchunguzi dhidi Teodoro kuhusu mali zake zinazokadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya dola milioni 70 huku akituhumiwa kutumia vibaya madaraka yake ya uwaziri katika serikali ya nchi hiyo.
Imeelezwa kuwa, wananchi wengi wa Guinea wanaishi maisha ya dhiki licha ya nchi hiyo kupata pesa nyingi kutokana na kuuza mafuta. Rais wan chi hiyo amedumu madarakani kwa zaidi ya miongo mitatu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment