KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 26, 2012

Equatorial Guinea yatinga robo fainali, Senegal nje

ABUBAKAR Suiuenei Obaidy (kushoto) wa Libya akigombea mpira na Rainford Kalaba wa Zambia timu hizo zilipomenyana juzi katika mechi ya kundi A ya michuano ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, iliyochezwa mjini Bata. Timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2.


BATA, Equatorial Guinea
WENYEJI Equatorial Guinea juzi walionyesha maajabu katika fainali za michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kuichapa Senegal mabao 2-1 katika mechi ya kundi A iliyochezwa mjini hapa.
Kipigo hicho kimeifanya Senegal, iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye fainali za mwaka huu, ifungashe virago mapema.
Ushindi huo uliiwezesha Equatorial Guinea kuwa timu ya kwanza kufuzu kucheza robo fainali ya michuano hiyo wakati timu nyingine ya kundi hilo itajulikana baada ya mechi za mwisho.
Mshambuliaji Kily ndiye aliyewapa furaha mashabiki wa Equatorial Guinea waliokuwa wamefurika uwanjani baada ya kuifungia bao la pili na la ushindi dakika za majeruhi.
Equatorial Guinea ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 62 lililofungwa na Randy, kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Kily.
Senegal ilisawazisha bao hilo dakika moja kabla ya mchezo kumalizika kupitia kwa Moussa Sow. Alifunga bao hilo kufuatia mpira wa adhabu uliopigwa na Niang.
Kutokana na matokeo hayo, ili ifuzu kusonga mbele, Senegal sasa italazimika kuishinda Libya katika mechi yake ya mwisho keshokutwa huku ikiomba dua Zambia ifungwe na Equatorial Guinea.
Senegal ndiyo timu pekee iliyokuwa ikiundwa na safi kali ya washambuliaji katika fainali hizo, lakini wameshindwa kuonyesha makali yao.
Ushindi wa Equatorial Guinea ulipokelewa kwa furaha kubwa na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Gilson Paulo, ambaye alikabidhiwa jukumu la kuinoa wiki tatu kabla ya kuanza kwa fainali hizo.
Katika mechi nyingine ya kundi hilo iliyochezwa juzi, Libya ilitoshana nguvu na Zambia baada ya kutoka sare ya mabao 2-2.
Pambano hilo halikuwa na mvuto kutokana na hali ya uwanja kutokuwa nzuri, kufuatia kujaa madimbwi ya maji baada ya mvua kunyesha kutwa nzima katika mji wa Bata.
Mechi hiyo ilichelewa kuanza kwa saa moja na Libya ilikuwa ya kwanza kuuzoea uwanja na kupata bao kupitia kwa mshambuliaji wake Ahmed Saad Osman.
Mchezaji huyo pia ndiye aliyeifungia Libya bao la pili kabla ya Ummanuel Mayuka kufufua uhai kwa Wazambia baada ya kufunga la kwanza na Christopher Katongo kusawazisha.
Kocha Mkuu wa Zambia, Herve Renard aliwashutumu maofisa wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa kuruhusu mechi hiyo ichezwe huku uwanja ukiwa umejaa maji.
“Nimesikitishwa sana kuona mwamuzi akiruhusu mchezo kuanza kwa sababu ilikuwa vigumu kucheza kwenye uwanja ukiwa katika hali hii,”alisema.
Renard alisema timu zote zilishindwa kuonyesha uwezo wake, badala yake mchezo ulikuwa wa kubutua na kukimbia badala ya kucheza soka.
Msimamo wa kundi A baada ya mechi za juzi ni kama ifuatavyo:
P W D L GF GA Pts

Eq. Guinea 2 2 0 0 3 1 6

Zambia 2 1 1 0 4 3 4

Libya 2 0 1 1 2 3 1

Senegal 2 0 0 2 2 4 0

No comments:

Post a Comment