KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, May 14, 2014

KABURU, JULIO WAJITOSA UCHAGUZI MKUU SIMBA






MAKAMU mwenyekiti wa zamani wa klabu ya Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' na aliyekuwa akikaimu nafasi yake, Joseph Itang'are 'Kinesi' wamechukua fomu za kuwania nafasi ya makamu wa rais.

Kujitokeza kwa Kinesi na Kaburu kuwania nafasi hizo, kumeufanya uchaguzi mkuu wa klabu hiyo unaotarajiwa kufanyika Juni 29 mwaka huu uwe mgumu zaidi.

Kinesi alichukua fomu juzi wakati Kaburu alichukua fomu jana huku akisindikizwa na kundi kubwa la wanachama.

Kocha Msaidizi wa zamani wa Simba,Jamhuri Kihwelu 'Julio' naye amejitokeza kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya makamu wa rais huku akitamba kuwa, ana uwezo mkubwa wa kushika wadhifa huo.

Julio aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa, anaifahamu vyema Simba na kuongeza kuwa, viongozi wengi waliowahi kuiongoza klabu hiyo ni wababaishaji.

Kinesi, Kaburu na Julio sasa watachuana na Sued Nkwabi na Badra Mayage katika kuwania wadhifa huo.

Katika nafasi ya rais, wagombea waliojitokeza hadi jana ni Evans Aveva, Michael Wambura na Andrew Tupa. Leo ndio siku ya mwisho kwa wagombea kuchukua na kurejesha fomu.

Kamati ya uchaguzi ya Simba inatarajiwa kukutana Mei 17 mwaka huu kwa ajili ya kuhakiki na kufanya mchujo wa wagombea. Majina ya wagombea watakaopitishwa yanatarajiwa kutangazwa Mei 19 mwaka huu.

Pingamizi kwa wagombea zitatolewa Mei 20 na 22 kabla ya kamati kuzipitia Mei 25 mwaka huu. Usaili kwa wagombea utafanyika Mei 29.

No comments:

Post a Comment