'
Friday, May 30, 2014
RAGE ATAKA SHERIA YA BMT IREKEBISHWE, AITAKA Z'BAR ISAHAU UANACHAMA WA FIFA, NKAMIA AMUONYA MALINZI KUBADILI JINA LA STARS
MWENYEKITI wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage ameikosoa Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na kutaka ifanyiwe marekebisho ili iendane na mabadiliko ya ulimwengu wa michezo.
Akichangia Bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo iliyowasilishwa Bungeni mjini Dodoma jana asubuhi, Rage alisema Sheria ya BMT imepitwa na wakati kwa sababu ina vitu vingi ambavyo vinavyozungumzia enzi za ujima ambazo kwa sasa havipo.
"Ipo Sheria ya BMT ya mwaka 1967 ambayo kwa mara ya mwisho ilifanyiwa marekebisho na Bunge mwaka 1971. Vitu vingi vilivyomo kwenye Sheria hiyo vimepitwa na wakati. Mfano, inazungumzia kuwania uongozi lazima uwe mwanachama wa TANU, chama ambacho kwa sasa hakipo," amesema Rage.
Aidha, Rage ametumiwa fursa hiyo kuwaomba wanachama na wapenzi wa Simba watulie kipindi hiki ambacho klabu hiyo iko katika mchakato wa uchaguzi mkuu.
"Ninawaomba wanachama wa Simba watulie katika kipindi hiki cha kusaka viongozi wapya ili masuala yote yanayohusu mchakato wa uchaguzi mkuu yashughulikiwe kwa misingi na taratibu zilizopo za mpira wa miguu," amesema Rage.
Katika hatua nyingine, Rage, ambaye pia ni mbunge wa Tabora Mjini (CCM) amelitaka BMT kuhakikisha linakuwa na kipengele katika Katiba yake inayokataza watu wanaopeleka masuala ya soka katika mahakama za kiraia.
"Ukiangalia Katiba za TFF, CAF na FIFA zinakataza masuala ya soka kuingiliwa na serikali na kupelekwa katika mahakama za kiraia. BMT iwe na kifungu cha sheria kinachokataza watu wanaopeleka masuala ya soka katika mahakama za kiraia ili iende sanjari na Katiba za mashirikisho hayo," amesema Rage.
Rage, ambaye anamaliza muda wake wa miaka minne wa kuiongoza Simba Juni 29, mwaka huu tangu aingie rasmi madarakani Mei 10, 2010, amewataka Wazanzibar kutopoteza muda wa kusaka uanachama FIFA kwa vile suala hilo ni sawa na ndoto za mchana.
"Wanachama wote wa FIFA, isipokuwa zile nchi maalum kisoka za Scoatland na Wales, ni wanachama wa UN (Umoja wa Mataifa). Zanzibar si mwanachama wa UN, hivyo hawezi kuwa mwanachama wa FIFA. Nimeamua kulisema hili mapema ili Waziri asisumbuke kuulizwa maswali juu ya hatua iliyofikiwa ya Zanzibar kusaka uanachama katika shirikisho hilo la soka la kimataifa," amesema zaidi Rage.
Wakati huo huo, serikali imelitaka Shirikisho la Soka nchini (TFF) kuachana na mpango wa kubadilisha jina la timu ya taifa (Taifa Stars) badala yake ijikite katika kuboresha kikosi cha timu hiyo.
Akijibu maswali ya wabunge leo asubuhi Bungeni mjini Dodoma, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia (pichani chini), amesema hakuna haja ya kubadili jina hilo kwa kuwa kufanya hivyo serikali haioni kama kutakuwa na mantiki.
"Tumepokea maoni ya TFF kutaka kubadili jezi za timu ya taifa kwa kuwa rangi ya bluu kwenye TV inaleta matatizo. Pia wamependekeza kubadili jina la timu ya taifa. Serikali inaona hakuna haja ya kubadili jina badala yake wajikite katika kubadili mchezo wenyewe," amesema Nkamia.
Mapema mwezi huu, Rais wa TFF, Jamal Malinzi alisema jijini Dar es Salaam kuwa watakusanya maoni ya Watanzania kupata jina jipya la timu ya taifa na aina ya jezi ambazo timu hiyo itakuwa inavaa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment