MSANII nyota wa filamu nchini, Rachel Haule 'Recho', amefariki dunia.
Recho alifariki dunia juzi katika hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bongo Movie, Steve Nyerere, alisema jana kuwa, Recho alipelekwa hospitalini hapo kwa ajili ya kujifungua.
Kwa mujibu wa Nyerere, msanii huyo alijifungua kwa njia ya upasuaji, lakini mtoto wake alifariki muda mfupi baadaye wakati hali ya msanii huyo ikiwa mbaya.
Alisema baada ya msanii huyo kuwa mahututi, alihamishiwa kwenye chumba cha uangalizi maalumu, lakini hali ilikuwambaya zaidi na kufariki dunia.
Alisema kifo cha msanii huyo ni pigo kubwa katika tasnia ya filamu nchini kwa vile kifo chake kimetokea siku chache baada ya kufariki kwa Adam Kuambiana.
"Hili ni pigo kubwa sana kwetu, lakini hatuna budi kumshukuru Mungu kwa kuwa yeye ndiye mwamuzi wa kila jambo. Tunachopaswa kufanya ni kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu,"alisema.
Recho alianza uigizaji mwaka 2009, akicheza maigizo katika kikundi cha Mburahati kabla ya kuanza kucheza filamu.
Alizaliwa mkoani Ruvuma katika wilaya ya Songea na kupata elimu ya msingi katika shule ya Luida iliyoko wilayani humo.
Miaka michache baadaye, alihamia Dar es Salaam na kujiunga na shule ya sekondari ya Baptist iliyoko Magomeni kabla ya kuhamia sekondari ya Hanga.
Baada ya kumaliza sekondari, alijiunga na Chuo cha Utumishi wa Umma cha Magogoni.
No comments:
Post a Comment