'
Wednesday, May 21, 2014
TAIFA STARS, ZIMBABWE ZAINGIZA MILIONI 63
Mechi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika mwakani nchini Morocco kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Zimbabwe iliyochezwa Jumapili katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 63,345,000.
Mapato hayo katika mechi hiyo iliyomalizika kwa Taifa Stars kuibuka na ushindi wa bao 1-0 yametokana na washabiki 11,079 waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 20,000.
Mgawo wa mapato hayo ni asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 9,662,796.61, gharama za kuchapa tiketi sh. 6,000,000, asilimia 15 ya uwanja ni sh. 7,152,330.51, asilimia 20 ya gharama za mchezo sh. 9,536,440.68 na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa pamoja wamepata sh. 30,993,432.20.
WASHABIKI KWENDA HARARE KUSHANGILIA STARS
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaandaa utaratibu utakaowawezesha washabiki kwenda jijini Harare, Zimbabwe kushuhudia mechi ya Taifa Stars.
Mechi hiyo ya marudiano ya Kombe la Afrika kwa ajili ya fainali zitakazochezwa Morocco mwakani itafanyika Jumapili (Juni 1 mwaka huu) jijini Harare.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ilishinda mechi ya kwanza iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwa bao 1-0.
Usafiri huo utakuwa wa basi ambapo washabiki wanatarajiwa kuondoka siku ya Ijumaa na kuwasili Jumapili mchana jijini Harare ambapo watashuhudia mechi na kuanza safari ya kurejea Dar es Salaam siku hiyo hiyo.
Washabiki wanatakiwa kuwa na hati za kusafiria (pasipoti), nauli ya kwenda na kurudi itakuwa sh. 300,000.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment