'
Monday, May 12, 2014
KOMREDI WAMBURA AJITOSA UENYEKITI SIMBA
Na Dina Ismail, Dar es Salaam
BAADA ya ‘memba’ wa kundi la Friends Of Simba (F.O.S), Evans Elieza Aveva jana kuchukua fomu ya kugombea Uenyekiti wa Simba SC, hasimu mkubwa wa kundi hilo, ‘Komredi’ Michael Richard Wambura naye leo amejitokeza kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo.
Wambura anayefanya idadi ya wagombea Urais wa Simba SC kufika watatu baada ya Aveva na Andrew Tupa, alifika makao makuu ya klabu majira ya saa tano na ushei asubuhi ya leo akisindikizwa na wafuasi wake, na kwenda kuchukua fomu hiyo.
Uchumi na timu bora; Komredi Wambura akisindikizwa na wafuasi wake kwenda kuchukua fomu leo
Wambura hakwenda kwa mbwembwe nyingi na msafara mkubwa kama ule uliomsindikiza Aveva jana na baada ya kuchukua fomu aliondoka zake.
Wambura ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Muda Simba SC mwaka 2006, ameingia na sera za kuinua uchumi wa klabu na kuboresha timu.
“Simba SC ina miaka zaidi ya 78, lakini hadi leo ipo kama SACCOS watu wanajichumia tu, wanaweka 100 wanachukua 200, mimi nataka kuleta mabadiliko, timu hii ijitegemee,”alisema.
Wambura aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) tangu enzi za FAT (Chama cha Soka Tanzania) kuanzia mwaka 2001 hadi 2004, amesema anataka kuijengea Simba SC uwezo wa kujitegemea.
“Nia ninayo, uwezo ninao na dhamira ninayo, na hayo nitadhihirisha nikiingia madarakani Simba SC,”alisema Wambura aliyewahi pia kuwa Mjumbe wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuanzia mwaka 1996 hadi 2005.
Jana wakati Aveva anakwenda kuchukua fomu alikuwa akionyesha vidole vitatu, akimaanisha pointi tatu kwamba sera yake ni ushindi- lakini akizungumza baadaye alisema atajitahidi kuleta mageuzi ya kiuchumi na kisoka kwa ujumla katika klabu hiyo, inayoifuatia Yanga SC kuzaliwa zaidi ya miaka 70 iliyopita. IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BIN ZUBEIRY
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment