KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, August 3, 2012

LIGI DARAJA LA KWANZA SASA TIMU 24

Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kuanzia msimu huu wa
2012/2013 itakuwa na timu 24 kutokana na mabadiliko ya
mfumo wa mashindano yaliyofanywa na Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Kamati ya Utendaji ya TFF ilikutana Julai 29 mwaka huu
ambapo pamoja na mambo mengine ilifanya mabadiliko
ya mfumo wa mashindano ikiwemo FDL kuchezwa kwa
mtindo wa nyumbani na ugenini badala ya ule wa awali
wa vituo.
Kutokana na mabadiliko hayo, timu za FDL zitagawanywa
katika makundi mawili ya timu 12 kila moja kutokana na
ukaribu wa kanda na kucheza kwa mtindo wa nyumbani
na ugenini.
Timu ya kwanza kutoka kila kundi itapanda kucheza Ligi
Kuu msimu unaofuata wakati ya tatu itakayoungana na
hizo mbili itapatikana kwa mechi za nyumbani na ugenini
kwa timu zilizoshika nafasi ya pili katika kila kundi.
Ili kufikisha idadi ya timu 24 kwenye FDL, Kamati ya
Utendaji ya TFF kwa kuzingatia mapendekezo ya Kamati
ya Mashindano imeamua timu tatu za juu kwenye Ligi ya
Taifa kutoka vituo vyote vitatu vya ligi hiyo zimepanda
daraja.
Sasa timu 24 za FDL ni Ashanti United (Dar es Salaam),
Burkina Moro (Morogoro), Green Warriors (Dar es
Salaam), Kanembwa JKT (Kigoma), Kurugenzi Mafinga
(Iringa), Majimaji (Ruvuma), Mbeya City (Mbeya), Mkamba
Rangers (Morogoro), Mlale JKT (Ruvuma) na Morani
(Manyara).
Nyingine ni Moro United (Dar es Salaam), Mwadui
(Shinyanga), Ndanda (Mtwara), Pamba (Mwanza), Polisi
(Arusha), Polisi (Dodoma), Polisi (Iringa), Polisi (Mara),
Polisi (Tabora), Rhino Rangers (Tabora), Small Kids
(Rukwa), Tessema (Dar es Salaam), Transit Camp (Dar es
Salaam), Villa Squad (Dar es Salaam)
Timu nne zitashuka daraja kurudi Ligi ya Mkoa. Timu hizo
ni mbili zilizoshika nafasi za mwisho kwa kila kundi. Timu
nne zitakazopanda kucheza FDL zitapatikana kwa mchujo
utakaohusisha mabingwa wa mikoa.
Kwa mfumo huo mpya wa mashindano, ligi za mikoa
zitakazosimamiwa na kuendeshwa na vyama vya mpira wa
miguu vya mikoa zinatakiwa kuwa na timu zisizopungua 16
na zisizozidi 20. Ligi za mikoa pia zitachezwa mwaka
mzima kwa mikondo miwili (nyumbani na ugenini).
Ligi ya mkoa itashusha timu mbili na kupandisha nyingine
mbili kutoka ligi ya wilaya. Ligi za wilaya zitakazosimamiwa
na kuendeshwa na vyama vya mpira wa miguu vya wilaya
zinatakiwa kuwa na timu zisizopungua 10 na zisizozidi 20.
Kwa wilaya zenye timu zaidi ya 20, chama husika cha
mpira wa miguu kitapanga utaratibu wa kuzichuja kwa
mashindano ili kupata zile bora 20 zitakazocheza ligi rasmi
ya wilaya.
Mabingwa wa wilaya katika mkoa husika watacheza mechi
za kuchujana (play offs) ili kupata timu mbili
zitakazopanda daraja kucheza ligi ya mkoa husika.
Kutokana na mabadiliko hayo ya mfumo wa mashindano,
sasa madaraja rasmi ya ligi ni Ligi Kuu, Ligi Daraja la
Kwanza, Ligi ya Mkoa (Ligi Daraja la Tatu) na Ligi ya
Wilaya (Ligi Daraja la Nne).
TFF inasisitiza kuwa kwa mujibu wa kalenda yake ya
matukio, kipindi cha usajili wa wachezaji kwa madaraja
yote ni kimoja, na ligi zitachezwa kwa wakati mmoja.
Usajili wa hatua ya kwanza ni kuanzia Juni 15 hadi Agosti
10 mwaka huu wakati kipindi cha pili cha usajili ni Agosti
21 hadi Septemba 4 mwaka huu. Usajili wa dirisha dogo ni
Novemba 15 hadi Desemba 15 mwaka huu.
Ligi kwa madaraja yote zitaanza Septemba. Ligi Kuu
itaanza Septemba Mosi mwaka huu, Ligi Daraja la Kwanza
ni Septemba 15 mwaka huu, Ligi ya Mkoa na ile ya Wilaya
zenyewe zitaanza Septemba 8 mwaka huu.
Mechi za kufungua msimu kwa madaraja yote (Ngao ya
Jamii) ambazo kwa sasa zinakutanisha bingwa na makamu
bingwa zitachezwa Agosti 25 mwaka huu wakati michuano
ya Kombe la FA itaanzia wilayani Septemba 24 mwaka
huu.

No comments:

Post a Comment