KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, August 5, 2012

SIMBA YASISITIZA YONDANI NI MALI YAO, YATAKA ILIPWE MIL 50/-



Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage amesisitiza kuwa, beki Kelvin Yondan aliyesajiliwa na klabu ya Yanga msimu huu bado ni mchezaji wao halali.

Rage amesema hayo leo wakati wa mkutano mkuu wa wanachama wa Simba uliofanyika kwenye ukumbi wa bwalo la maofisa wa polisi, Oysterbay mjini Dar es Salaam.

Rage alisema Yanga imemsajili beki huyo kinyume na kanuni kwa vile alishatia saini makubaliano ya kuongeza mkataba wake na Simba.

Alisema iwapo Yanga inamtaka mchezaji huyo, inapaswa kuilipa Simba shilingi milioni 50, vinginevyo hawawezi kumruhusu aichezee katika ligi kuu ya Tanzania Bara msimu ujao.

"Hatuna shida sana na Yondan, lakini lazima taratibu zifuatwe, hivyo kama wanataka kuvunja mkataba wake, lazima watulipe milioni 50," alisema Rage.

Yondan amejiunga na Yanga baada ya kulipwa kitita cha sh. milioni 30 na pia atakuwa akilipwa mshahara wa sh. milioni moja kwa mwezi.

Mara baada ya Yanga kutangaza kumsajili mchezaji huyo, Simba iliwasilisha malalamiko yake kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa madai kuwa, usajili huo ni batili.

Hata hivyo, TFF iliyatupilia mbali malalamiko hayo ya Simba na kumruhusu Yondan kuichezea Yanga katika michuano ya Kombe la Kagame iliyomalizika hivi karibuni mjini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment