Kiungo Ramadhani Chombo Redondo amesema yeye ni mchezaji halali wa Simba kwa vile mkataba wake na Azam ulishamalizika tangu Juni mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Redondo alisema ameamua kujiunga na Simba kwa vile kwa sasa yeye ni mchezaji huru.
Redondo amesajiliwa na Simba kwa kitita cha sh. milioni 30, ambapo tayari ameshalipwa sh. milioni 20 wakati sh. milioni 10 zingine atalipwa baadaye.
"Ninavyojua ni kwamba mkataba wangu na Azam ulishamalizika tangu Juni mwaka huu na sikuwa na mpango wa kuongeza mkataba mwingine,"alisema.
Kwa mujibu wa Redondo, baada ya uongozi wa Azam kumsimamisha kwa miezi minne mapema mwaka huu kwa tuhuma za utovu wa nidhamu, alielezwa kwamba ataongezewa mkataba iwapo ataonyesha mabadiliko kitabia na uwanjani.
"Lakini siku zimekuwa zikienda bila kuelezwa lolote na uongozi wa Azam hadi mkataba wangu umemalizika ndio sababu nimeamua kujiunga na Simba,"alisema.
Mwenyekiti wa Azam, Nassor Idrissa alisema jana kuwa, hawana taarifa kuhusu kusajiliwa kwa Redondo katika klabu ya Simba na kusisitiza kuwa, anachotambua ni kwamba bado ni mchezaji wao halali.
"Kama Simba walikuwa wanamtaka mchezaji huyo, walipaswa kufuata taratibu kama walivyofanya kwa Mrisho Ngasa,"alisema mwenyekiti huyo.
Hata hivyo, habari kutoka ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zimeeleza kuwa, ni kweli mkataba kati ya Azam na Redondo umemalizika na kwamba kwa sasa ni mchezaji huru.
Mmoja wa viongozi waandamizi wa TFF amesema leo kuwa, Simba haipaswi kulaumiwa kumsajili mchezaji huyo kwa vile yupo huru na Azam wameshindwa kumuongeza mkataba mwingine.
Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange Kaburu hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo jana kwa madai kuwa, watalitolea maelezo wakati utakapofika.
No comments:
Post a Comment