KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, August 7, 2012

OKWI ATUA DAR, ATULIZA PRESHA SIMBA

Mshambuliaji Emmanuel Okwi ameshusha presha ya mashabiki na wanachama wa klabu ya Simba baada ya kutua nchini leo akitokea nchini Uganda.
Okwi alitua kwenye uwanja wa ndege wa Dar es Saam leo jioni kwa ndege na Shirika la Ndege la Uganda na kupokewa na baadhi ya viongozi wa Simba, akiwemo Makamu Mwenyekiti, Geofrey Nyange Kaburu.
Kuwasili kwa Okwi kulishusha presha waliyokuwa nayo wana Msimbazi baada ya kuwepo na taarifa kwamba Yanga ilikuwa ikimuhitaji mchezaji huyo kwa udi na uvumba.
Baadhi ya vyombo vya habari viliripoti juzi kuwa, mjumbe wa kamati ya utendaji ya Yanga, Abdalla Bin Kleb alikwenda Uganda mwishoni mwa wiki iliyopita kwa lengo la kumshawishi Okwi ajiunge na timu hiyo.
Okwi alirejea Uganda wiki iliyopita akitokea nchini Austria, ambako alikwenda kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa katika klabu ya Red Bull Salzburg.
Imeelezwa kuwa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uganda amefuzu majaribio hayo na anatarajiwa kurejea huko wakati wowote.
Akizungumzia ujio wa mchezaji huyo, Kaburu alisema Okwi anatarajiwa kuichezea Simba katika mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Nairobi City itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kaburu alitoa onyo kwa viongozi wa Yanga kuacha kumfuatafuata mchezaji huyo kwa vile bado ana mkataba na Simba na ni kinyume cha sheria kufanya naye mazungumzo kabla ya kuwasiliana na uongozi.
Makamu Mwenyekiti huyo alisema kitendo cha viongozi wa Yanga kumfuatafuata Okwi ni sawa na kutapa tapa baada ya kupigwa bao katika vita ya kumsajili beki Mbuyi Twite kutoka APR ya Rwanda.
Mechi kati ya Simba na Nairobi City ni sehemu ya tamasha la Simba, ambalo litatumika kuwatambulisha wachezaji wapya wa klabu hiyo na pia kuwapa tuzo viongozi waliotoa michango mbali mbali kwa klabu hiyo.

No comments:

Post a Comment