KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, August 8, 2012

NGASA, REDONDO, OKWI LAIVU SIMBA DAY

Mshambuliaji Emmanuel Okwi akipokea tuzo ya mwanasoka bora wa msimu wa 2011/12 kutoka kwa mmoja wa wadhamini wa klabu hiyo, Profesa Phillemon Sarungi.


Shomari Kapombe akipokea tuzo ya mchezaji mwenye nidhamu kutoka kwa Profesa Sarungi.




Klabu ya Simba leo imetoa tuzo kwa wanamichezo wake katika tamasha la kila mwaka la Simba Day lililofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Katika tuzo hizo, marehemu Patrick Mafisango alipewa tuzo ya heshima, Shomary Kapombe
alitwaa tuzo ya mchezaji mwenye nidhamu wakati Emmanuel Okwi alipewa tuzo ya
mchezaji bora wa klabu hiyo kwa msimu uliopita.


Watu wengine waliotwaa tuzo ni mwanachama wa siku nyingi wa klabu hiyo, Professa Philemon Sarungi, ambaye alipewa tuzo ya kuwa mtu aliyetoa mchango wa muda mrefu katika klabu hiyo, Haidari Abeid maarufu kama Muchacho alitwaa tuzo ya mchezaji wa bora wa Simba wa miaka ya 70's, Hamisi Kilomoni - mchezaji bora wa miaka ya 60 na Ally Sykes akapata tuzo ya heshima na udhamini.


Wakati wa tamasha hilo, washambuliaji Emmanuel Okwi, Mrisho Ngasa na Ramadhani Chombo Redondo walikuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki wa Simba kutokana na kushangiliwa kwa mayowe mengi.

Tamasha hilo lilianza saa 9.15 alasiri kwa utambulisho wa wachezaji, ambapo Redondo aliyesajiliwa na Simba wiki hii akitokea Azam FC, alikuwa wa mwisho kutambulishwa kwa mashabiki na kushangiliwa kwa nguvu.

Okwi aliyewasili nchini juzi akitokea Uganda baada ya kufanyiwa majaribio katika klabu ya Red Bull Salzburg ya Austria, naye alishangiliwa kwa mayowe mengi kutokana na taarifa zilizokuwepo awali kwamba klabu ya Yanga ilikuwa ikimuwinda kwa udi na uvumba.

Baada ya utambulisho huo wa wachezaji, Simba ilitambulisha jezi zake mpya itakazotumia katika msimu ujao wa ligi kupitia kwenye luninga kubwa iliyopo kwenye uwanja huo. Jezi hizo zenye rangi nyekundu na nyeupe, zilikuwa na majina ya wachezaji wa timu hiyo.

Akizungumza wakati wa utambulisho huo, Kamwaga alisema jezi hizo zitaanza kuuzwa kwa mashabiki kwa utaratibu maalumu na aliwaonya mashabiki kuepuka kununua jezi feki.

Kamwaga alisema Simba itaanza kutumia jezi hizo katika mechi yake ya kuwania Ngao ya Hisani dhidi ya Azam, inayotarajiwa kuchezwa Agosti 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mwendelezo wa tamasha hilo, Simba ilichapwa mabao 3-1 na Nairobi City Stars katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa kwenye uwanja huo.


Kufungwa huko kwa Simba kulitokana na kocha Milovan Cirkovick kubadilisha karibu kikosi kizima kilichoanza na kuingiza wachezaji wapya, ambao waliitoa City Stars ya Nairobi nyuma kwa 1-0 na kuipa ushindi wa 3-1.


Simba ilitangulia kupata bao kupitia kwa Felix Sunzu dakika ya 15, pasi ya Mwinyi Kazimot na ilikwenda kupumzika ikiwa mbele kwa bao hilo, lakini kipindi cha pili, kipa aliyempokea Juma Kaseja, Hamadi Waziri alitunguliwa mabao matatu katika dakika 57 na Duncan Owiti, dakika ya 64 na Bruno Okullu na dakika ya 79 na Boniphace Onyango.


No comments:

Post a Comment