KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, November 2, 2011

Yanga yaipumulia Simba



SIMBA jana iliitibulia Yanga uwezekano wa kumaliza ligi hiyo ikiwa kileleni, baada ya kuilazimisha Moro United kutoka nayo sare ya mabao 3-3 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Mshambuliaji Salum Machaku ndiye aliyeinusuru Simba isiadhirike baada ya kuifungia bao la kusawazisha dakika ya 81 na kuifanya iambulie pointi moja.
Moro United itabidi ijilaumu kwa kushindwa kutoka uwanjani na ushindi kwani ilishawaweka mashabiki wa Simba roho juu baada ya kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 3-1.
Kwa matokeo hayo, Simba imemaliza mechi za mzunguko wa kwanza ikiwa kileleni kwa tofauti ya pointi moja kati yake na Yanga, ambayo jana iliichapa Polisi Dodoma bao 1-0.
Simba imemaliza mzunguko huo ikiwa na pointi 28 baada ya kucheza mechi 13 huku ikiwa imefunga mabao 21 na kufungwa manane.
Yanga imeshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 27 baada ya kucheza mechi 13, ikiwa imefunga mabao 20 na kufungwa tisa.
Iliwachukua Moro United dakika mbili kuhesabu bao la kwanza kupitia kwa Andrew Kasembe baada ya kuunganisha wavuni mpira wa krosi kutoka pembeni ya uwanja.
Simba ilisawazisha dakika ya 22 kwa bao lililofungwa kwa kichwa na Obadia Mungusa kabla ya Moro United kuongeza la pili dakika ya 43 kupitia kwa Kasembe, aliyewalamba chenga mabeki wawili pamoja na kipa Juma Kaseja.
Gaudence Mwaikimba aliifungia Moro United bao la tatu dakika ya 45 baada ya mabeki wa Simba kuzembe kumkaba. Timu hizo zilikwenda mapumziko Moro United ikiwa mbele kwa mabao 3-1.
Gervas Kago aliiongezea Simba bao la pili dakika ya 76 kwa shuti kali la mbali baada ya kupokea pasi kutoka kwa beki Juma Jabu.
Salum Machaku aliisawazishia Simba dakika ya 81 kwa bao la mpira wa adhabu, uliokwenda moja kwa moja wavuni huku mabeki wa Moro United na kipa wao, Lucheke Mussa wakiwa wameduwaa.
Moro United ililazimika kumaliza mchezo huo ikiwa na wachezaji 10 baada ya beki wake wa kulia, Salum Telela kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumchezea rafu mbaya Jonas Gerrard wa Simba.
Pambano hilo nusura liingie doa wakati wa mapumziko baada ya baadhi ya mashabiki wa Simba kutaka kuvamia ndani ya uwanja kwa lengo la kuwapiga wachezaji wao, wakiwatuhumu kucheza chini ya kiwango.
Ilibidi polisi wa kutuliza ghasia waingilie kati kwa kuwazuia mashabiki hao wasiingie ndani ya uwanja na hivyo kuifanya hali iwe shwari.
Kadhalika Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange alijikuta akiwa kwenye wakati mgumu baada ya baadhi ya wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kumtolea lugha chafu.
Moro Utd: Lucheke Mussa, Salum Telela, Jaffer Gonga, Rajabu Zahir, Tumba Swedy, Omega Seme, Geofrey Wambura, Yahya Sharif/Rajabu Tahir, Gaudence Mwaikimba/Omari Gayo, Lambele Reuben, Andrew Kasembe/Bakari Mpakala.
Simba: Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Juma Jabu, Obadia Mungusa, Juma Nyoso, Mwinyi Kazimoto/Gervas Kago, Patrick Mafisango, Ulimboka Mwakingwe/Jonath Gerrard, Felix Sunzu, Haruna Moshi, Salum Machaku.
Wakati huo huo, Yanga imemaliza mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo kwa ushindi baada ya kuichapa Polisi bao 1-0 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri.
Bao pekee na la ushindi la Yanga lilifungwa na mshambuliaji, Kenneth Asamoah dakika ya 44.

1 comment: