KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, November 2, 2011

Siwezi kumsahau baba-Osita


LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu machachari wa Nigeria, Osita Iheme amesema bado ana huzuni kubwa ya kufiwa na baba yake mzazi tangu akiwa mdogo na amekuwa akimjia ndotoni mara kwa mara.
Akihojiwa na gazeti la Entertainment Express la Nigeria hivi karibuni, Osita alisema baba yake alifariki mwaka 1990 katika mazingira ya kutatanisha.
Osita, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Ukwa alisema, wakati wa kifo hicho, alikuwa bado mdogo mno kiumri, hivyo hana kumbukumbu nzuri.
Hata hivyo, Osita alisema siku ya kifo chake, ilimjia ndoto usingizini kuhusu kifo hicho na alipowaeleza ndugu zake, walishangaa kwa sababu kilishatokea.
“Tulikuwa tukiishi Aba, lakini baba yangu akifia kijijini kwetu. Siwezi kusema mimi ni mtu wa miujiza, lakini Mungu anazo njia zake za kuwasiliana nami kupitia kwenye ndoto,”alisema Osita, ambaye amecheza filamu zaidi ya 50.
“Siwezi kuzungumza mengi kuhusu yeye kwa sababu wakati anafariki, nilikuwa bado mdogo. Nilichokuja kubaini baadaye ni kwamba, alikuwa mfanyabiashara aliyekuwa akisafiri mara kwa mara, akiuza bidhaa mbalimbali,”alisema.
“Alikuwa akihakikisha kwamba, watoto wake wanakua vizuri. Alitupa malezi mazuri na kutufundisha kumwabudu Mungu. Alikuwa baba wa aina yake,”aliongeza.
Kwa mujibu wa Osita, saa chache kabla ya kifo chake, baba yao, ambaye alikuwa kiongozi katika jamii yao, aliaga kwamba anakwenda kijijini kwao, lakini siku iliyofuata, wakapelekewa taarifa kwamba amefariki.
Osita alisema yeye ndiye aliyerithi tabia ya kujiamini aliyokuwa nayo baba yake, ambaye amemwelezea kuwa, alikuwa na akili nyingi na aliweza kumkabili yeyote na kumweleza kosa alilofanya bila kumwogopa.
Mcheza filamu huyo alisema, kutokana na kufiwa na baba yake tangu akiwa mdogo, alipata malezi makubwa kutoka kwa mama yake, ikiwa ni pamoja na kujifunza mengi kutoka kwake.
“Kila kitu kinachoonekana katika mwonekano wangu, nimekipata kutoka kwa mama yangu. Alikuwa na majukumu mengi kwetu, kutulisha na mengineyo,” alisema.
“Nilisikitika kumkosa baba kwa sababu nakumbuka hadithi nilizokuwa nikisimuliwa na kaka yangu jinsi alivyokuwa akiwafundisha kuwa na nidhamu. Kwa upande wake, mama hakuwa mkorofi,”aliongeza.
Osita alisema siku moja kabla ya kifo cha baba yake, ilimjia ndoto, ambapo alimuota akiwa amekufa na amekuwa akimjia ndotoni mara kwa mara
Alipoulizwa anamudu vipi kejeli kutoka kwa watu mbalimbali kuhusu umbile lake, Osita alisema kamwe huwa hajali na kuyapa uzito yale watu wanayoyasema kuhusu yeye.
Osita alisema anatarajia kufunga ndoa hivi karibuni, lakini bado hajapata mchumba na hajui karata hiyo itamwangukia nani.
“Ninachoweza kusema ni kwamba, wapo wengi pichani, ninaowafikiria. Lakini nikiwa mwanaume kijana, ninaye mmoja ninayemfikiria,”alisema.
Osita ni mmoja wa waigizaji bora wa kizazi chake nchini Nigeria. Amejipatia umaarufu mkubwa kutokana na kucheza filamu nyingine akiwa na Chinedu Ikedieze.
Mwaka 2007, mcheza filamu huyo alishinda tuzo ya mwigizaji bora wa AMAA. Osita anachukuliwa kuwa ni mmoja wa waigizaji maarufu zaidi nchini Nigeria.

No comments:

Post a Comment