KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, November 2, 2011

PAPIC: Nimerejea Yanga na mambo mapya


SWALI: Uongozi wa klabu ya Yanga umekurejesha kwa ajili ya kuinoa timu hiyo. Je, una jambo gani jipya kwa ajili ya Yanga?
JIBU: Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kurejea kuifundisha Yanga. Nimerudi na mambo mengi mapya, ikiwa ni pamoja na kukiimarisha kikosi cha Yanga ili kiweze kufanya vizuri katika michuano ya ligi na kimataifa.
Lakini kazi hiyo itakamilika vizuri iwapo nitapata ushirikiano mkubwa kutoka kwa uongozi, wanachama na mashabiki wa Yanga.
Unajua mafanikio katika mchezo wa soka yanaanzia kwenye maandalizi, ambalo ni jukumu la uongozi kuhakikisha timu inaingiza kambini na huduma kwa wachezaji zinakuwa nzuri. Pia kukiwa na umoja, lazima mambo yaende vizuri.
SWALI: Ulipoondoka Yanga, kocha mwenzako, Sam Timbe aliiwezesha kutwaa ubingwa wa bara na kombe la kagame. Umejipanga vipi katika kuendeleza rekodi hizo?
JIBU: Nampongeza sana kocha huyu kwa kuipa ubingwa Yanga. Naweza kusema ameniachia changamoto moja kubwa kwamba, ni lazima nihakikishe ubingwa unaendelea kubaki Yanga.
Vilevile ninakabiliwa na jukumu zito la kukisuka kikosi cha Yanga ili kiweze kufanya vizuri katika michuano ya klabu bingwa Afrika baada ya kutolewa mapema msimu uliopita.
Ninachokifanya kwa sasa ni kuangalia kasoro zilizopo kwenye kikosi changu ili niweze kuzifanyiakazi, hasa katika usajili wa dirisha dogo.
Nitaangalia ni sehemu zipi katika timu zenye udhaifu ili niweze kutoa taarifa kwa uongozi na kutafuta wachezaji wa kuongeza nguvu.
SWALI: Kuna malalamiko kutoka kwa mashabiki wa Yanga kwamba, baadhi ya wachezaji waliosajiliwa msimu huu uwezo wao ni mdogo na mchezaji anayetajwa zaidi ni David Mwape. Una maoni gani kuhusu malalamiko haya?
JIBU: Unajua watu wengi hawafahamu umuhimu wa Davies Mwape. Kwangu mimi ni mchezaji muhimu sana na ambaye anaweza kuwachosha mabeki wa timu pinzani.
Anapokuwa uwanjani, Mwape anakuwa na kazi maalumu na ndio maana nilimsajili msimu uliopita kwa ajili ya kuongeza nguvu katika ushambuliaji na aliweza kupachika mabao mengi.
Bado nina imani mchezaji huyu ataweza kuisaidia Yanga kwenye michuano ya ligi kuu msimu huu na hata klabu bingwa Afrika.
Lakini napenda kuwaeleza mashabiki wa soka wa Tanzania wabadilike kwa vile soka hivi sasa ina mabadiliko makubwa sio kama zamani.
Siyo siri kwamba, inanibidi nifanye kazi ya kusajili baadhi ya wachezaji wapya ili timu yangu iweze kuendelea kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali.
Nitasajili wachezaji watatu wa ndani ya nchi ili niweze kupata matokeo mazuri zaidi. Suala la kusajili wachezaji kutoka nje kwa sasa halipo akilini mwangu.
SWALI: Mwishoni mwa wiki iliyopita, uliingoza Yanga kuifunga Simba bao 1-0 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara. Nini siri ya mafanikio haya?
JIBU: Nilijua wazi kwamba lazima utaniuliza swali hili. Napenda kuwapongeza wapenzi wote wa Yanga, wachezaji pamoja na viongozi kwa ushindi huu.
Siri ya ushindi huu ni kuwepo kwa umoja miongoni mwa viongozi, wanachama na wachezaji na huu ndio uliochangia kupatikana kwa matokeo hayo mazuri.
Iwapo viongozi na wanachama wataendelea kushikamana kama ilivyo sasa, nina hakika Yanga itaendelea kuifunga Simba kwa miaka mingi zaidi. Umoja ni muhimu sana.

1 comment: