KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, November 9, 2011

ALI AMLILIA FRAZIER




PHILADELPHIA, Marekani
BINGWA wa zamani wa ndondi za uzani wa juu duniani, Muhammad Ali amesema kifo cha Joe Frazier kimeifanya dunia impoteze bondia aliyeweka historia ya aina yake katika mchezo huo.
Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu Frazier alipofariki dunia, Ali amemwelezea mwanamasumbwi huyo kuwa alikuwa bingwa wa kweli wa ndondi hizo.
Frazier (67) alifariki dunia Jumatatu iliyopita kwa ugonjwa wa kansa ya ini, ambao ulikuwa ukimsumbua kwa muda mrefu na kumfanya alazwe hospitali na kuwekwa chini ya uangalizi maalumu.
Ali alizipiga na Frazier mara tatu miaka ya 1970, ambapo alipigwa katika pambano la kwanza na kushinda mapambano mawili yaliyofuata.
Mbali na Ali, watu wengine mbalimbali wametuma salamu za rambirambi kutokana na kifo cha Frazier, ambaye wakati wa uhai wake, alipachikwa jina la Smokin’Joe.
Hata hivyo, ujumbe uliogusa hisia za mashabiki wengi wa ndondi hizo ni ule uliotolewa na Ali, ambaye mapambano yake matatu dhidi ya Frazier yataendelea kukumbukwa daima.
Ali na Frazier walizipiga kwa mara ya kwanza mwaka 1971 mjini New York na kurudiana katika mji huo huo miaka mitatu baadaye kabla ya kuzipiga tena mjini Manila mwaka 1975.
“Dunia imempoteza bingwa wa aina yake. Siku zote nitamkumbuka Joe kwa heshima zote,” ilisema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Ali kuhusu kifo hicho.
Frazier alikuwa na chuki na Ali kwa miaka mingi baada ya wote wawili kustaafu ndondi hizo, kufuatia Ali kutoa kauli nyingi za kumbeza.
Hata hivyo, vita yao ya maneno ilimalizika miaka michache baadaye, kufuatia kila mmoja kumsamehe mwenzake na kuungana katika kuelezea kumbukumbu za mapambano yao enzi za ujana wao.
Bingwa mwingine wa zamani wa ndondi hizo, Lennox Lewis wa Uingereza amemwelezea Frazier kama bondia, ambaye hajawahi kutokea na kwamba aliweka historia ya aina yake.
“Mchango wake katika mchezo huu hauelezeki na hauwezi kusahaulika,”alisema Lennox. “Atakosekana, lakini kamwe hatosahaulika.”
Salamu zingine za rambirambi zilitoka kwa watu mbalimbali maarufu, wakiwa ndani na nje ya mchezo wa ndondi, zikionyesha jinsi Frazier alivyokuwa akizigusa nyoyo zao.
Promota wa ndondi hizo, Frank Warren alisema mapambano kati ya Ali na Frazier na lile dhidi ya George Foreman yanadhihirisha kwamba, bondia huyo atakumbukwa kama mwanamichezo wa aina yake.
Frazier aliiwezesha Marekani kutwaa medali ya dhahabu katika michezo ya Olimpiki ya mwaka 1964 iliyofanyika Tokyo, Japan kabla ya kujitosa katika ndondi za kulipwa.
“Alikuwa sehemu ya mapambano bora ya dunia, ambayo hayajawahi kutokea,”alisema Warren.
“Watu wanazungumza kuhusu Mike Tyson alipokuwa na umri wa miaka 21. Vyema, Joe Frazier alipokuwa kijana, alikuwa bondia mzuri kama yeye kama si zaidi ya Tyson,”aliongeza Warren.
Bondia Floyd Mayweather Jr alisema, dunia imempoteza bondia wa kihistoria wakati Oscar de la Hoya alisema: 'Nitakukosa rafiki yangu.'
Frazier alikuwa bondia wa kwanza kumdunda Ali baada ya kumwangusha chini katika raundi ya 15 katika pambano kati yao lililofanyika kwenye ukumbi wa Madison Square Garden mwaka 1971.
Baada ya pambano hilo, Ali alizungumza maneno mengi ya kumponda Frazier, lakini bingwa huyo wa zamani aliamua kumsamehe.
Siku chache kabla ya kifo chake, Frazier alikaririwa akisema kuwa, ameamua kusahau yale yote yaliyotokea miaka ya nyuma na kwamba amemsamehe Ali kwa kila alichokisema.
“Huwezi kumtaja Ali bila kumtaja Joe Frazier,” alisema mwandishi wa ngumi katika shirika la habari la AP, Ed Schuyler. “Alimpiga Ali, usisahau hilo.”
Mabondia hao wawili, walipigana kwa zaidi ya raundi 41 na katika pambano lao la mwisho lililofanyika nchini Philippines, walirushiana makonde mazito huku Frazier akionekana kuongoza hadi raundi ya 14.
Hata hivyo, ilipofika raundi ya 15, Frazier alizidiwa na kushindwa kuona sawa sawa, hali iliyosababisha kocha wake, Eddie Futch amwelekeze kusalimu amri.
Nje ya ulingo, Ali alikuwa akitoa lugha ya dhihaka kwa Frazier, akimwita gorilla. Lakini alimuheshimu kama bondia bora, hasa baada ya Frazier kushinda pambano lao la kwanza kwa pointi na kuweka rekodi ya kuwa bondia wa kwanza kumdunda Ali. Pambano hilo lilimwezesha kila bondia kulipwa dola milioni 2.5 za Marekani.
Pambano hilo lililopigwa miaka 40 iliyopita, liliendelea kubaki kwenye kumbukumbu ya Frazier kila alipokuwa akizungumzia maisha yake, kazi yake na uhusiano wake na Ali. Alizungumza hayo kwa mara ya mwisho miezi michache kabla ya kifo chake.
“Hicho kilikuwa kitu cha aina yake, ambacho kamwe hakikuwahi kutokea katika maisha yangu,”alisema Frazier alipohojiwa na AP.
Frazier alitwaa ubingwa wa dunia kwa mara ya kwanza mwaka 1970 baada ya kumdunda Jimmy Ellis walipozipiga kwenye ukumbi wa Madison Square Garden.
Ubingwa wake huo ulidumu katika pambano manne yaliyofuata, likiwepo alilomdunda Ali, kabla ya kupata kipigo kutoka kwa Foreman mwaka 1973, ambaye alimwangusha mara tatu katika raundi ya kwanza na mara tatu nyingine katika raundi ya pili.
Katika mapambano mengine mawili yaliyofuata, Frazier alidundwa na Ali katika raundi ya 12 na baadaye alifanikiwa kumdunda Foreman waliporudiana nchini Zaire (sasa DRC).

No comments:

Post a Comment