KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, November 9, 2011

TIMBE: Nitarudi Yanga


ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Yanga, Sam Timbe amesema hana deni na klabu hiyo na kwamba anatarajia kurejea nchini wakati wowote na kuendelea kuifundisha timu hiyo.
Timbe alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita, saa chache kabla ya kupanda ndege kurejea kwao Uganda.
Kocha huyo aliyeziwesha timu tatu tofauti za Afrika Mashariki na Kati kutwaa Kombe la Kagame, aliondoka nchini kwa ndege ya Kenya Airways.
Timbe alisema anaushukuru uongozi wa Yanga kwa kuweza kumlipa fedha zote alizokuwa akiidai klabu hiyo baada ya kuvunja mkataba wake.
Hata hivyo, Timbe hakuwa tayari kutaja fedha alizolipwa, lakini habari kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, amelipwa zaidi ya sh. milioni 30.
“Sijutii kukatishwa mkataba wangu, hiki ni kitu cha kawaida kwetu, leo naondoka, lakini kesho naweza kurudi kama Papic (Kostadi-kocha wa sasa Yanga),”alisema.
Timbe alisema anashukuru kwa ushirikiano mzuri alioupata kutoka kwa baadhi ya viongozi na wachezaji wa timu hiyo na kusisitiza kuwa, anaondoka bila ya kuwa na kinyongo na mtu yeyote.
Uongozi wa Yanga uliamua kukatisha mkataba wa Timbe kwa madai kuwa, alikuwa haelewani na wachezaji na pia alikuwa akikataa kufuata maagizo ya mabosi wake.
Kocha huyo alitoa usia kwa mchezaji chipukizi wa Yanga, Idrisa Rajabu, akimtaka awe mwangalifu na kuzingatia mafunzo ya makocha kwa vile ana kipaji cha juu cha uchezaji soka.
Alisema kutokana na umri wake mdogo, Idrisa ana uwezo wa kucheza soka kwa miaka mingi na kwa kiwango cha juu iwapo atafuata miiko ya mchezo huo.
“Idrisa ni kijana mdogo, aepuke kuzungumza sana na vyombo vya habari, asilewe sifa mapema, namtabiria atakuwa nyota baadaye,”alisema.

No comments:

Post a Comment